Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi amewataka wanufaika wa mikopo ya 10% kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwapa nafasi wanufaika wengine kukopa kwa ajili ya kukuza biashara zao kwa maslahi yao na Taifa.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru amesema hayo Aprili 17, mwaka huu wakati wa kuona kituo cha Enlight development organisation (EDO) kinachowawezesha vijana kiuchumi na kupinga ukatili kwa watoto kilichopo Halmashauri ya Mji Ifakara Wilayani Kilombero.
Akifafanua zaidi, Ndugu Ismail amesema mikopo hiyo isiyokuwa na riba imetengwa kwa ajili ya vijana, watu wenye ulemavu pamoja na wanawake ili kukuza vipato vyao hivyo, amewataka wanaochukua mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili wahitaji wengine waweze kukopa.
"... vijana wanaokopeshwa fedha wanatakiwa wazirejeshe ili wengine waweze kutumia fedha hizo..." amesema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Katika hatua nyingine, amelipongeza dawati la jinsia kwa kufanya kazi kwa haki na kwa ufanisi mkubwa hivyo amewataka wataalam hao kuhakikisha wananchi wanaoshinikizwa na vitendo vya unyanyasaji wanasimamiwa na kupata haki yao ili kuondoa vitendo hivyo kuendelea ndani ya jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo cha EDO Bi. Josephine Saidi amesema kituo hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wanawake wa hali ya chini wanaokumbana na changamoto ya maisha pamoja na ukatili wa kijinsia hivyo kituo hicho kinawapa mafunzo ya kilimo cha mbogamboga na matunda ili kupata uwezo wa kwenda kujitegemea kiuchumi.
Naye, mnufaika wa mradi huo Bi. Makrina Raphael ameishukuru serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan kuwapa mkopo wa Tsh. Mil.10 inayotokana na fedha za 10% huku akiahidi kuzirejesha kabla ya mkataba wao wa miaka 2 kumalizika.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.