Wananchi wa Kijiji cha Rose kata ya Magomeni Wilayani Kilosa wameeleza kuhusu mafanikio walioyapata kupitia mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ambapo wamebainisha kuwa mfuko huo umewatoa kutoka katika hali duni ya umaskini wa kupindukia hadi kufikia hali ya wastani wa kuweza kupata mahitaji muhimu ya siku yakiwemo chakula, malazi na mavazi.
Wananchi hao wamesema hayo Januari 27, Mwaka huu wakati wa ziara ya viongozi wa TASAF kutoka Makao Makuu wakiongozwa na Mkurugenzi wa Miradi ya TASAF hapa nchini Bw. John Steven walipofanya ziara katika Kijiji cha Rose Kata ya Magomeni Wilayani Kilosa kwa lengo la kukagua miradi ya TASAF iliyotekelezwa Wilayani humo.
Wakielezea mafanikio hayo, wananchi wa Kijiji cha Rose Kata ya Magomeni akiwemo Bi. Dorothea Mbombwe amesema baada ya kubahatika kuwa mnufaika wa TASAF, fedha alizozipata zimemsaidia katika masomo na kuhitimu elimu ya Stashahada ya maendeleo ya jamii na kuiomba serikali kuendelea kusaidia kaya zinazokidhi vigezo ili nao waweze kuondokana na umaskini wa kupindukia.
"...kwenye suala la TASAF napenda kuishukuru kwa sababu imenisaidia kwenye suala zima la elimu mpaka hapa nilipofikia ngazi ya stashahada ya elimu ya maendeleo ya jamiii..." amesema Bi. Dorothea
Naye, Bi. Lilian Samwel kutoka kata hiyo ameishukuru Serikali kwa kuanzisha Mradi wa TASAF kwani amesema Mfuko huo umemsaidia kununua chereheni kinachomsaidia kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha familia yake ya kila siku.
Mkurugenzi wa Miradi ya TASAF Taifa Bw. John Steven amesema, TASAF imeweza kufanikisha miradi mingi ndani ya Mkoa wa Morogoro yenye thamani ya sh. Bil. 66, kati ya hizo zimetolewa kwa njia ya mtandao wa simu na kupitia benki, huku akieleza uwepo wa ajira za muda zikizotolewa ambapo zimetumia kiasi cha Tsh. Bil. 23 na kutekeleza miradi 1500 Mkoani humo .
Bw. John amebainisha mafanikio mengine makubwa yaliyofanyika Mkoani humo kuwa ni pamoja na kuwafikia walengwa 43000 kati yao 21000 wamehitimu katika mpango wa TASAF na kuunda vikundi zaidi ya 3000 vikiwa na wanachama zaidi ya 36000 katika hivyo vikundi vimeweza kupatiwa kiasi cha Ths. Mil. 522 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za vikundi vyao.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Morogoro Bw. Jacob Kayange amesema moja ya masharti kwa walengwa wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni kuhudhuria kliniki kwa kupitia mpango wa ruzuku wa TASAF, hivyo amesema Mkoa huo umefanikiwa kwa 98% ya watoto walengwa kupelekwa kliniki na 89.3 % kwenda shule za msingi na sekondari na kwa sababu hiyo mpango wa TASAF umefanikisha watoto wa kaya masikini kwenda shule na kliniki.
Timu hiyo ya viongozi wa TASAF kutoka Makao makuu ikiongozwa na Mkurugenzi wa Miradi ya TASAF hapa nchini, leo imetembelea mradi wa mfereji wa maji wenye kingo za kuzuia mafuriko kwa makazi ya kijiji cha Rose, vikundi vya wanachama mbalimbali ambao ni wanufaika wa TASAF ambapo Wilayani humo ina walengwa 8,900 kati ya hao wanachama 2000 wameweza kuhitimu katika mpango huo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.