Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa, amewasisitiza waratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi wa Wizara na Mikoa kuhakikisha wananchi wanawezeshwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo zinazoinufaisha jamii.
Katibu Mtendaji huyo amesisitiza hayo wakati akifungua kikao cha NEEC na Waratibu wa Uwezeshaji ngazi ya Wizara na Mikoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Edema iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kikiwa na lengo la kukumbushana majukumu mbalimbali ya kazi na mafunzo kwa waratibu wapya.
Akifafanua zaidi, Bi. Beng’i Issa amesema wananchi wanapaswa kuhusishwa katika shughuli za kiuchumi za Taasisi, Wizara na Mikoa ili kuwawezesha kuwa na umiliki wa miradi hiyo, ikiwemo ya ujenzi, mikopo na mafunzo mbalimbali ya kuwaongezea ujuzi kwa ajili ya manufaa yao.
"...kazi kubwa wanayotakiwa kufanya waratibu katika maeneo yao ni kuhakikisha uwezeshaji wa wananchi unajitokeza katika shughuli za Wizara, Taasisi na Mikoa..." Amesema Katibu Mtendaji huyo.
Sambamba na hayo, Bi. Beng’i amesema Serikali ina program ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) inayolenga kuboresha utoaji wa mikopo ya 10% katika Halmashauri, uboreshaji wa uwezo wa kuingia katika manunuzi ya umma 30%, pamoja na kuangalia vipaumbele vya Mkoa husika na ushiriki wa wananchi katika shughuli mbalimbali zilizopo katika jamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoani Morogoro, Dkt. Rozalia Rwegasira, ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mkoani humo, amesema katika Mkoa huo kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika hususan kilimo, biashara na ujenzi wa miradi ya maendeleo, ambapo hutoa kipaumbele kwa wazawa ili kukuza uchumi wao na wa Mkoa kwa ujumla.
Naye, Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoani Kilimanjaro, Bw. James Bwanali, amesema kupitia kikao hicho cha kujengeana uzoefu, hasa mafanikio waliyoyapata Mkoa wa Morogoro katika kuimarisha uchumi wa wananchi wengi kupitia program ya IMASA, ili kwenda kuitekeleza katika Mikoa yao.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.