Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo ya mfumo mpya wa - NeST Bw. Leopold Ngirwa akitoa mafunzo kwa washiriki wa mafunzo hayo.
NeST, ni Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma yaani National - e - Procurement System, mfumo ambao umeundwa na wazawa hapa nchini. Mfumo huo unaotarajiwa kuwa mbadala wa mfumo wa awali wa manunuzi ya Umma uliojulikana kama Tanzania National e Procurement System yaani TANePS.
Mwishoni Julai 31 hadi Agosti 4 mwaka huu, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma – PPRA, ilianza rasmi kutoa mafunzo ya kwa wataalamu ngazi ya mikoa namna ya kutumia mfumo wa NeST, wataalamu sita kwa kila Mkoa wa Tanzania Bara.
Wataalamu hao walikuwa na jukumu la kuujua vema mfumo huo na kisha kwenda kufundisha Maafisaengine ndani ya mikoa yaani Halmashauri zote zilizopo katika Mkoa husika.
Mkoani Morogoro tayari Timu hiyo ya Wataalamu sita kutoka Sekretarieti ya Mkoa huo imekwisha tekeleza jukumu lake la msingi kwa kutoa mafunzo ya mfumo wa NeST kwa wataalamu 62 waliotoka Halmashauri zote tisa za Mkoa huo.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mbaraka Mwinshehe Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kufunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Utumishi Bw. Herman Tesha Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa yalianza Agosti 28 yamehitimishwa Septemba Mosi huku akisisitiza washiriki kwenda kuwa wakufunzi kwa wengine mara warejeapo katika Halmashauri zao.
Washiriki nao waliusifu mfumo huo na kwamba una tija kubwa kwa watanzania;
Kwanza, wakitoa pongezi kwa Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuwaendeleza watanzania na kuwaamini kuunda mfumo wa NeST.
Pili, kwa kuwa mfumo huo wa NeST umeundwa na wazawa wenyewe kuna uhakika wa asilimia kubwa mfumo utaongeza usiri na usalama kwa nyaraka za Serikali ukilinganisha na mfumo wa TANeMPS uliokuwa chini ya wageni.
Tatu, mfumo huu pia umeelezwa kuwa ni mfumo wa wazi kwa kuwa kila mchakato wa manunuzi ya Umma utakaofanyika ndani ya mfumo, kila aliyepewa dhamana ya kuingia kwenye mfumo huo atakuwa anaona au kujua kinachoendelea humo hivyo kupunguza changamoto ya rushwa wakati wa mchakato wa kutangaza zabuni.
Nne, mfumo huu utapunguza gharama kubwa ikiwemo matumizi ya karatasi (Paper Works) Kwa kuwa mchakato wa ununuzi wa umma na utangazaji wa zabuni kwa kiasi kikubwa utatumika ndani ya mfumo.
Mkaguzi wa Ndani wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Steven Benedict akitoa mafunzo kwa washiriki wa mafunzo hayo ya mfumo mpya wa Manunuzi - NeST.
Akifunga mafunzo hayo, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Ofisi hiyo Bw. Herman Njelekela amewataka washiriki kwenda kuanza mara moja kuwafundisha wataalamu wengine kwa kuwa mfumo wa TANeMPS utazimwa ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na Mfumo wa NeST kuunza kutumika.
Afisa Tehama kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Njelekela akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa NeST wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Washiriki wa mfumo wa NeST nao walipata fursa na kuishukuru Serikali kwa kuleta mfumo huo na kwamba utaleta chachu katika utendaji kazi wa Serikali na kurahisisha shughuli za ununuzi hivyo kuharakisha kuleta maendeleo ya wananchi hususan katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Pamoja na kutoa pongezi hizo kwa Serikali juu ya mfumo mpya wa NeST, walikuwa na maoni kwa serikali:
Bw. Hosam Issale (Mhasibu) Halmashauri ya Ulanga anasema ili mfumo wa NeST ufanye kazi ipasavyo viongozi wanaotakiwa kuingia kwenye mfumo huo wawe wepesi kukasim mamlaka yao kwa waliochini yao wanapokuwa hawana nafasi, hii itasaidia kuondoa ucheleweshaji wa mchakato ndani ya mfumo huo, vinginevyo mfumo huo utakuwa hauna manufaa kama inavyo tazamiwa na changamoto ya manunuzi kuchukua muda mrefu itabakia palepale.
Lakini pia Bw. Issale anasema mfumo huu Pamoja na uzuri wake wa kuwa mfumo wa wazi na unaotekelezeka haraka lakini unategemea sana mtandao, hivyo anaishauri Serikali kuimarisha zaidi Mtandao mahali mfumo ulipo lakini pia katika halmashauri husika.
Naye Bw. Nkwabi Simon (Mhandisi) Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ameusifu mfumo wa NeST kuwa unapunguza gharama.
Aidha, Mhandisi Nkwabi maoni yake kwa PPRA ni kuhakikisha mfumo wa NeST unatumika kwenye matumizi ya fedha zinazopitia force Account ili kuokoa fedha nyingi za Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia Forse Account.
Serikali imeshatoa maelekezo kuwa mfumo wa TANePS utazimwa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu na mfumo wa NeST utaanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu, huku ikiwataahadharisha Wakuu wa taasisi kutofanya manunuzi yoyote ya umma nje ya mfumo wa NeST na watakaokwenda kinyume cha maagizo hayo watachululiwa hatua kali za kinidhamu.
Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya mfumo mpya wa Manunuzi - NeST wakielezea uelewa wao kuhusu mfumo huo baada ya kupatiwa mafunzo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.