Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa kwenye kikao cha kutoa taarifa ya utekelezaji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema watu watakaofanya makazi au shughuli zozote za kimaendeleo katika ardhi oevu ya Dakawa Wilayani Mvomero eneo ambalo imegundulika kuwa kuna chanzo cha maji hawatapata fidia yoyote.
Mhe.Fatma Mwassa amesema hayo februari 23, mwaka huu wakati wa kikao cha kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akitoa taarifa ya sekta ya maji Mhe. Fatma Mwassa amesema pamoja na Serikali kuanza utekelezaji wa kuboresha Bwawa la maji la Mindu na Ujenzi wa Bwawa la Kidunda bado Mkuu huyo wa Mkoa ametaja chanzo kingine cha maji kutoka eneo la dakawa na kuwataka wananchi kutofanya shughuli zozote za kijamii katika eneo hilo.
Aidha, inaelezwa kuwa eneo hilo la Dakawa ndilo lenye maji mengi na tosherevu kwa ajili ya Manispaa na maeneo jirani huku akibainisha kuwa kwa sasa eneo hilo linakabiliwa na changamoto ya watu kulivami huku akitoa tahadhari kwa wananchi kutojenga wala kufanya shughuli za kibinadamu na atakayekwenda tofauti na maagizo hayo Serikali haitatoa fidia yoyote kwake.
“... changamoto sasa watu wameanza kuvamia na kuanza kujenga, niwaombe ndugu zangu kupitia kikao hiki hakuna hata mtu mmoja anayekwenda kujijengesha kwenye chanzo cha maji, tutabomoa nyumba kavu kavu kwani wananchi wameshaambiwa lakini hawataki kusikia...”
Amesema, tatizo la maji Morogoro litakuwa historia baada ya kukamilisha ukarabati wa bwawa la mindu na kuchimba visima Dakawa kwani serikali imetoa Tsh. 185,000,000 kwa ajili ya kukarabati ili kuongeza ujazo wa maji na kuongeza chujio katika bwawa hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Joseph Masanga amesema kuna miradi ya maji ambayo haijakamilika hivyo viongozi wanatakiwa kushirikiana ili kukamilisha miradi hiyo na kutatua tatizo la maji.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Solomon Kasaba amesema kamati ya siasa kupitia kikao kilichokwisha fanyika kuna mambo yanatakiwa kufanyiwa mageuzi ikiwa ni matumizi ya fedha zinapelekwa kama sadaka, fedha za serikali zinatolewa kwa watu hewa, kamati imekaa na kuamua kuchukua hatua kwa watu hao.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.