Wananchi wa Mtaa wa Mtawala Kata ya Mwembesongo Mkoani Morogoro wametakiwa kuacha mila potofu dhidi ya jaribio la Sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Septemba 11 mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Sensa Kitaifa Bi. Anne Makinda Septemba Mosi mwaka huu alipokuwa anazungumza na wananchi wa kata hiyo kwa lengo la kuwafahamisha umuhimu unaotokana na zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Bi. Anne amebainisha kuwa, watu wengi wamekuwa na imani potofu juu ya zoezi la Sensa ya watu na makazi hali ambayo hupelekea baadhi yao kujiweka mbali na zoezi hilo kila inapotokea kufanyika.
‘’Hatufanyi Sensa kwa ajili ya Siasa, chama wala kwa dini yoyote isipokuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya watanzania’’ amesema Makinda.
Aidha, Makinda amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa viongozi watakaokuja kuhesabu kaya zao na kusaidia kujibu maswali ambayo yameorodheshwa katika madodoso ya Sensa.
Sambamba na hayo, Makinda amesema iwapo zoezi la Sensa na makazi litafanyika vizuri litaisaidia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kutambua matumizi bora ya kodi zinazotolewa na wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema Mkoa wa Morogoro umejipanga vizuri katika zoezi zima la Sensa ya watu na makazi na tayari wameshafanya uteuzi wa kamati kwa ajili ya zoezi hilo.
Licha ya uteuzi wa kamati hizo, Shigela ameeleza kuwa hadi sasa kamati hiyo imeshatambua idadi ya kaya kwenye vijiji, vitongoji na mitaa yote ili kurahisisha zoezi la kuhesabu watu muda utakapofika.
‘’…Lakini pia tumeweza kuwa na namba za mawasiliano za viongozi wa maeneo hayo. kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji ili kurahisisha shughuli za Sensa akiwa amepangiwa kitongoji fulani hatuhangaiki kutafuta mawasiliano yao’’ amesema Shigela.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi kwa upande wa Mipango na Uratibu Anza Amen Ndossa ambaye pia ni Mratibu wa Sensa Mkoa wa Morogoro amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi hilo kwa lengo la kuwa na Sensa itakayoleta ufanisi na matokeo chanya kwa Taifa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.