WATANZANIA TUPENDE MCHEZO WA GOFU - DKT. NDUMBARO
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. DAMAS Ndumbaro ametoa wito kwa watanzania wote kupenda michezo hasa mchezo wa golfu kutokana na mchezo huo kuwa mzuri na ni rafiki kwa kila mtu na kwa kila rika katika kuucheza.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo Mei 4, 2024 wakati wa kuhamasisha mchezo huo wa golfu Mkoani Morogoro akiwa ameambatana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima na viongozi wengine wa Serikali ngazi ya Mkoa.
"....Watanzania wote tuipende michezo na mchezo wa golfu ni mmoja kati ya michezo ambayo hauchagui umri mtu yoyote kwa umri wowote anacheza.." amesema Waziri Damas Ndumbaro.
Akisisitiza zaidi amesema kuwa wanamorogoro wana bahati, kwa Mkoa kuwa na viwanja viwili vya golfu ambavyo ni kiwanja cha Gymkana kilichopo Manispaa ya Morogoro na kiwanja cha Kilombero.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam kighoma Malima amesema watahakikisha kila shule inakuwa na viwanja vya michezo ili watoto wanaposoma waweze kupata ujuzi wa michezo mbalimbali na kukuza vipaji vyao.
Mhe. Malima amebainisha kulipokea agizo la Waziri na kawmba wataenda kulifanyia kazi kwa kila Halmashauri za Mkoa wa Morogoro na kuratibu kila shule iwe na viwanja vya michezo na kuweka katika mizania baina ya michezo ya watoto wakike na wakiume.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa huo una viwanja bora vya golfu, lakini havitumiki ipasavyo na wenyeji wake, hivyo amewataka wanamorogoro kujifunza mchezo wa Golfu na sio kusubiri watu kutoka nje waje kuvitumia viwanja hivyo vya Gymkana na Kilombero.
Katika hatua nyingine Mhe. Malima amesema kutakuwa na mashindano ya Golfu (Morogoro Open) yatakayofanyika Juni 14, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo na June 17 Waziri wa Michezo atafunga mashindano hayo, nivyo ameomba wachezaji wote wa kitaifa na kimataifa kuhudhuria mashindano hayo.
Naye Meya wa Manipsaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amesema ni kama bahati na neema kwa Morogoro, Mji unaotarajia kuwa Jiji siku za usoni huku akifurahishwa naSerikali ya awamu ya sita kwa kitendo cha kuteua uwanja wa mpira wa CCM Morogoro kuwa miongoni mwa viwanja vitakavyofanyiwa maboresho makubwa lakini pia Mkoa wa Morogoro kupewa heshima ya kuwa na shule ya kwanza ya kuibua vipaji mbalimbali vya michezo
"... Sisi kama Manispaa tumekubali na tupo tayari kutoa hiyo shule na cha pili tupo tayari kutoa kiwanja kama wapo tayari kujenga .." amesema Mhe. Kihanga.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.