Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka watendaji wa Serikali kuwajibika katika nafasi zao wanazozitumikai kwa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi na huku akiwatahadharisha kuwa serikali ya awamu ya sita haitomfumbia macho mtendaji yeyote ambaye hatoendana na kasi ya serikali iliyopo madarakani.
Daniel Chongolo amesema hayo Februari 5 mwaka huu kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama hicho yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro.
Katibu Mkuu huyo amesema, haiwezekani Serikali itoe fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi halafu wale wenye dhamana ya kutatua changamoto hizo hawatimizi wajibu wao.
“...tunachotaka kuona ni kila kilicho ahidiwa na kikatolewa fedha na Serikali, fedha ile inaenda kuleta matokeo ya kubadilisha maisha ya mwananchi na sio maneno na hadithi..” amesema Daniel Chongolo.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa inapunguza mfumuko wa bei hapa nchini.
Waziri Bashe amesema ili kufikia hatua hiyo serikali ni kuanza kununua mazao kutoka kwa wakulima na kuyahifadhi katika maghara ya Serikali ambapo mpaka sasa tayari wamehifadhi tani 23 za mahindi, na kwamba Serikali itawauzia wananchi wake kwa bei ya shilingi 700 kwa kilo.
Aidha, ameogeza kuwa Serikali imetoa tani 247,000 za mbolea za ruzuku kwa ajili ya kuleta tija kwenye kilimo na kuongeza uzalishaji.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa salamu za Mkoa ameishukuru Serikali ya CCM kwa kutekeleza kwa vitendo ilani ya chama hicho kwa kuwaondolea kero mbalimbali wanamorogoro ikiwemo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama maji, barabara, umeme pamoja na kutatua migogoro ya ardhi na ile ya wakulima na wafugaji.
Maadhimisho hayo ya kuzaliwa kwa CCM yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, Katibu wa Itikadi na Uenezi Bi. Sofia Mjema, Katibu wa Organization na Siasa, mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Sekta za Maji, Ardhi, Mifugo na Uvuvi, Tamisemi na Kilimo, Wabunge wa Mkoa wa Morogoro, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wananchi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.