Mkoa wa Morogoro umedhamiria kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watendaji wote wa Serikali watakaojihusisha na uuzaji wa Ardhi bila kufuata taratibu, kanuni, miongozo na sheria za nchi lengo likiwa ni kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya Ardhi iliyoshamiri Mkoani humo.
Uamuzi huo umefikiwa Januari 24 mwaka huu wakati wa kikao kazi cha viongozi na watendaji wa MKoa wa Morogoro wa ngazi ya Mkoa na Wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kikao ambacho kiliongozwa na Mkuu wa MKoa huo Mhe. Fatma Abubakar Mwassa.
Katika kikao hicho hoja nyingi ziliibuliwa na kujadiliwa ikiwaa ni pamoja na kukithiri kwa migogoro ya Ardhi ambapo ilielezwa kuwa baadhi ya viongozi wa Vijiji na Kata na Wenyeviti wa Vijiji wamehusishwa kuwa ndio chanzo kikuu cha changamoto hiyo kwa kuuza ardhi bila kufuata taratibu, miongozo, kanuni na sheria zilizopo.
“... kijiji na mkutano wake hauna uwezo wa kuuza ardhi kwa muwekezaji zaidi ya heka 50.....kwa hiyo ninyi viongozi mtusaidie kutatua mgogoro huo, kwa sababu huo utakuwa ni utapeli”. Amesema Mhe. Paul Ngwembe Jaji Mfawidhi Kanda ya Morogoro.
Katika hatua nyingine wajumbe wa kikao hicho wamefikia kauli ya pamoja kuwa Soko la mazao ya viungo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro lifanyiwe ukarabati kutokana na kuliweka soko hilo katika hali nzuri zaidi ili kuwanufaisha wakulima zaidi ya 2,000 waliopo ndani ya Wilaya hiyo.
Maazimio mengine waliyokubalina katika kikao hicho ni pamoja na kuondoa vibanda vyote vya mbao vinavyozunguka Soko la Chifu Kingalu katika Manispaa ya Morogoro kuwa vibanda hivyo vinaharibu taswira ya soko hilo pamoja na kuhatarisha soko lenyewe endapo ikitokea hitilafu ya moto.
Katika kujizatiti kutekeleza miradi ya maendeleo, kikao kimeagiza Halmashauri zote za Mkoa huo zihakikishe hadi kufikia Juni 2023 fedha zote za miradi ya maendeleo ziwe zimetumika kwa kumalizia miradi husika ikiwa ni pamoja na kujenga miradi ya muda mrefu na yenye tija kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa masoko na utengaji wa maeneo ya kufanyia biashara ndogo.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho na ndiye aliyeitisha kikao hicho, akiwasilisha mada iliyohusu Dira ya Mkoa huo amesema, kazi kubwa ya Sekretarieti ya Mkoa ni kuimarisha Utawala Bora ili kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoa huduma bora na za kiwango cha juu katika maeneo yao.
Aidha, Mhe. Fatma Mwassa amesema kila Wilaya ihakikishe inakuwa na Mpango kabambe wa utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi ambapo mpango huo ndio utakuwa mwongozo katika kuyafikia maendeleo ndani ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla.
Kikao hicho kililenga kutathmini na kujadili maendeleo ya Mkoa huo, hususani kuangalia mafanikio, changamoto na namna ya kutatua hizo changamoto na kuja na mikakati ya kuboresha miundombinu itakayosaidia kukuza uchumi katika Mkoa huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.