Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Best Richard Magoma, amewataka wazazi na walezi kote nchini kuwapeleka watoto wanaodhaniwa kuwa wana meno ya plastiki, vimeo virefu, na tatizo la udata katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata matibabu ya kitaalamu badala ya kuendeleza mila potofu ya kuwapeleka watoto hao kwa waganga wa jadi.
Dkt. Magoma ametoa Wito huo Machi 12, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya kutoa elimu kwa jamii dhidi ya ukatili wa ukeketaji wa viungo vya kinywa kwa watoto wachanga uzinduzi uliofanyika Hoteli ya Glonency Manispaa ya Morogoro.
Amesema, magonjwa hayo ya watoto yanatibika katika vituo vya afya, hivyo ni jukumu la kila mtu kulinda haki za mtoto hao huku akiwataka wazazi na walezi kuachana na dhana potofu ya kuwapeleka watoto kwa waganga wa jadi, kwani kufanya hivyo ni moja ya matendo ya ukeketaji na ni ukatili kwa watoto.
"Napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza Watanzania wote kuwapeleka watoto wetu wanaodhaniwa kuwa na meno ya plastiki, kimeo kirefu, udata, na changamoto nyingine za kinywa katika vituo vya afya," amesema Dkt. Best Magoma.
Aidha, Dkt. Magoma amesema programu hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya 1,428, walimu wa afya mashuleni 1,327, kamati za maendeleo za kata, viongozi wa madhehebu ya dini 442, wahudumu wa afya ngazi ya jamii 2,101, pamoja na waganga wa tiba asili 450.
Ameongeza kuwa programu hiyo imeanza katika Mkoa wa Morogoro na itaendelea kwa kushirikiana na kamati za Usalama ngazi ya mkoa na wilaya ili kuwajengea uwezo maafisa hao katika kulinda afya za watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kinywa na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Baraka Nzobo, amesema wizara imejipanga kutokomeza tatizo hilo, hivyo amewataka wanaofanya shughuli za tiba asili wawe ni wale tu waliosajiliwa na Bodi ya Tiba Asili ili kufuata miiko na matakwa ya sheria katika utoaji wa tiba.
Aifha ameongeza kuwsWizara inalenga kutoa elimu kwa waganga wa jadi wanaotoa tiba zisizo rasmi ambazo zina madhara kwa watoto na kuonya kuwa wale watakaopuuza elimu hiyo na kuendelea na vitendo vinavyokiuka mafunzo, watakabiliwa na hatua kali za kisheria ili kukomesha ukatili huo kwa watoto.
Naye Rais wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania (TDA), Dkt. Gemma Berege, ametoa wito kwa wataalamu wa tasnia ya afya ya kinywa na meno kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii juu ya dhana potofu zinazoathiri watoto. Pia amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya afya ya kinywa na meno.
Kwa upande wake, mdau kutoka Shirika la Sibaba Dental Clinic, Dkt. Nilla Jackson, ambaye amefadhiliwa na Shirika la Bridge 2 Aid, amesema kuna umuhimu wa kushirikisha kamati za usalama katika kulinda afya ya kinywa na meno ya mtoto ili kusaidia kukomesha vitendo vya ukeketaji kwa watoto wadogo nchini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.