Watoto 423,000 walio chini ya Miaka mitano wanatarajiwa kupata chanjo ya Polio Mkoani Morogoro ili kuwakinga na ugonjwa huo, hii ni baada ya kupatikana kwa taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Malawi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Mei 18 mwaka huu wakati akizindua chanjo ya Polio kwa Watoto walio na umri chini ya miaka mitano Mkoani humo, zoezi ambalo limefanyika katika Viwanja vya Kituo cha Afya cha Sabasaba Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni ishara ya jitihada za Serikali za kuwalinda Watoto wa umri huo hapa nchini ili wasipate maambukizi na mashambulizi hatari ya Ugonjwa wa Polio.
Akiongea na hadhara iliyokuwepo katika viwanja hivyo, Martine Shigela amewataka Wazazi Mkoani humo kuhakikisha Watoto wao wanapata chanjo hiyo kwani Serikali imejipanga vema kupitia Watendaji wa ngazi zote kuhakikisha wanapita kila Kaya yenye Watoto walio chini ya Miaka mitano wanapatiwa chanjo hiyo.
“Mkoa wetu umejipanga kuchanja zaidi ya watu 423,000 na Wataalamu wetu wamejipanga vizuri kuhakikisha kila Familia yenye Mtoto ‘under five’ chini ya Uongozi wa watendaji wetu wa Mitaa, vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji na Wenyeviti wa Vijiji wanatembela Familia hizo na watoto hao wanapatiwa chanjo ya matone...” amesema Shigela.
Katika hatua nyingine Martine Shigela amebainisha kuwa mara ya mwisho Ugonjwa huo ulibainika nchini Tanzania Mwaka 1996, hivyo, kufanyika kwa uzinduzi wa chanjo hiyo leo, haina maana kwamba ugonjwa huo umeingia nchini kwetu la hasha, bali Serikali imefikia hatua hiyo ili kuchukua tahadhari baada ya taarifa za uwepo ugonjwa huo katika nchi jirani ya Malawi.
Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Paschal Kihanga amewapongeza wazazi wa Watoto wanaoishi katika Manispaa hiyo kwa hamasa walioionesha ya kuwapeleka watoto kupata chanjo ya Polio katika kituo hicho cha Afya.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio ameweka wazi kuwa Ugonjwa wa Polio hauna dawa na mara nyingi huwaathiri watoto wa umri huo na kupelekea ulemavu wa kudumu kwa mtoto na kwamba huambukiza kama yanavyoambukiza magonjwa mengine ya kuhara, hivyo amewataka wanajamii wajitokeze kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwani chanjo hiyo ni salama.
Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya Centers for Diseases Control and Prevention (CDC) Bw. Philip Talboy amesema kuwa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wanajamii wenyewe kwa kushirikiana pamoja, kutawezesha kukomesha na kuondoa na kuuondoa Ugonjwa wa Polio ndani ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.