Kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio kwa watoto chini ya miaka mitano inatarajia kuwafikia watoto zaidi ya 84941 katika Mkoa huo ambapo chanjo hiyo itatolewa kuanzia Disemba 1 hadi 4 mwaka huu, hivyo wazazi wametakiwa kushiriki kikamilifu.
Hayo yamebainishwa Novemba 28 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando katika kikao kilichoandaliwa na Idara ya Afya kwenye ukumbi wa Soko la Chifu Kingalu uliopo Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema chanjo hiyo ni salama na itatolewa kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwaka sifuri hadi miaka mitano.
“... na sasa tuone namna bora ya kutekeleza zoezi hili kwa ufanisi zaidi, kwa kuwa Mhe. Rais tayari ametimiza wajibu wake hivyo ni wajibu wa wazazi kuwatoa watoto kupatiwa chanjo ya polio”. amesema Mhe. Albert Msando.
Aidha, Mhe. Albet Msando amesisitiza kuwa ugonjwa wa polio hauna tiba lakini unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo ya matone ya polio.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya ametumia kikao hicho kuwahamasisha wazazi katika Mkoa huo kushiriki kikamilifu kwa kuwatoa watoto wao kupata chanjo hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando akiongea na wahudumu wa afya kwenye kikao kilichoandaliwa na Idara ya Afya.
Kwa upande wake Mratibu wa chanjo Manispaa ya Morogoro Dkt. Felista Rushimabahizi amesema zoezi hilo la utoaji wa chanjo hiyo ya polio litafanyika nyumba kwa nyumba ili kuwafikia watoto wengi zaidi, hivyo wazazi watoe ushirikiano kwa timu za wachanjaji zitakazopita kwenye nyumba zao ili kufanikisha zoezi hilo.
watoa huduma ya chanjo ya matone ya polio wakiwa kwenye utekelezaji wa kampeni ya nyumba kwa nyumba kutoa chanjo ya polio.
Zoezi hilo la utoaji wa chanjo hapa nchini linalenga kuwafikia watoto zaidi ya milioni 14, 490, 597 na timu za watoa chanjo hiyo watapita kila nyumba ili kuwapata watoto wengi.
Taarifa ya maendeleo ya kampeni ya chanjo kwa halmashauri za Mkoa wa Morogoro kwa siku tatu tangu kuanza kwa kampeni hiyo.
Taarifa hiyo ya chanjo kwa siku tatu tangu kuaza kwa kampeni hiyo imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watoto 552,958 wamepata chanjo katika Mkoa huo sawa na asilimia 87.30 huku zoezi hili bado linaendelea ndani ya Mkoa huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.