Watu wawili wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa Mkoani Morogoro kutokana na vurugu zilizozuka baina ya jamii ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Lubasazi, Kata ya Kolero, Wilayani Morogoro.
Tukio hilo limetokea Novemba 15, mwaka huu majira ya asubuhi baada ya kundi la watu 40 wakiwa na silaha za jadi kuvamia kambi ya wafugaji katika kitongoji cha kivumba.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Fotunatus Musilim amewataja waliofariki dunia kutika vurugu hizo kuwa ni Pamoja na Saito Molinge (50) na Salum Sambigu (40) wote ni wakazi wa kitongoji cha Sangasanga, kata ya Mvuha Wilaya ya Morogoro.
Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Morogoro wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa maagizo kwa Kamati hizo.
Aidha, Kamanda Musilim amesema chanzo cha tukio hilo ni wafugaji kuhamia eneo la wakulima kitendo ambacho kilipingwa na wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao ni wakulima hivyo kuamua kuwashambulia kwa lengo la kuwaondoa.
Sambamaba na hilo Kamanda Musilim amesema Jeshi la Polisi Mkoani humo tayari limechukua hatua ya kufika eneo la tukio na kukutana na pande zote mbili za wafugaji na wakulima kwa lengo kutuliza vurugu hizo.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amemuagiza Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro akishirikiana na Baraza la Madiwani la Wilaya hiyo kuwafuta kazi Mara moja Mtendaji wa Kijiji Pamoja na Mwenyekiti wake wa Kijiji cha Lubasazi kwa kutuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji ili waingize mifugo katika eneo hilo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akiwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama wakati wa kujadili tukio la kutafuta suluhu ya kudumu ya mauaji hayo.
Sambamba na agizo hilo amewataka wakulima kutojichukulia Sheria mikononi kwenye matukio Kama hayo badala yake watoe taarifa kwenye mamlaka husika na wafugaji kutochungia mifugo wao kwenye mashamba au maeneo ya Wakulima.
"...kwanza nitamke hakuna mwananchi anayeruhusiwa kuchukua sheria mkononi ya kuua mwengine eti kwa sababu kaingia mahali Fulani, sheria mkononi hairuhusiwi, na kwa sababu hiyo tuliowakamata jana watafunguliwa mashitaka...” amesema Fatma Mwassa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amesema atasimamia maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kufafanua kuwa watendaji ambao watashindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa huo akiwemo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akiongea na Kamati za Ulinzi na Usalama.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.