Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuwalea watoto katika misingi iliyo bora na sahihi ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Mhe. Malima ametoa wito huo Oktoba 11, Mwaka huu wakati wa uzinduzi wa kampeni maalum ya "Waambieni kabla hawajaharibiwa" iliyofanyika katika viwanja vya Kikosi cha Polisi cha Kutuliza Ghasia Tanzania (FFU) vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema wazazi na walezi wanajukumu la kuhakikisha wanatoa malezi yaliyo bora kwa watoto ili waweze kutimiza ndoto zao ambapo kampeni hiyo inatarajiwa kuwafikia vijana wa ngazi zote za elimu.
"...Ni jukumu la kila mzazi na kila mlezi kuwa ni sehemu ya kuwajibika katika kuhakikisha kwamba watoto wanapata malezi yanayo waelekeza kuandaa kesho yao ambayo ni bora zaidi.." amesema Mhe. Adam Malima
Pia Mhe. Malima amesema katika kampeni hiyo itaenda sambamba na kutoa elimu juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuongeza ujuzi katika masomo na kuondokana na kuiga tabia zisizofaa za mitandaoni hususan matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, mapenzi katika umri mdogo, ukatili wa kijinsia, wizi na ujambazi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amewataka watendaji wa Mkoa huo wa idara ya elimu wakiwemo Maafisa elimu wa shule za msingi na Sekondari, Wakurugenzi wa Halmashauri, kuhakikisha kuwa wanashirikiana vyema na Jeshi la Polisi kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya kikatili katika jamii.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.