Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amewataka wazazi, walezi, walimu na viongozi wote wa Serikali Mkoani Morogoro kushirikiana katika kuimarisha malezi na maadili mema kwa watoto katika Mkoa huo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo Mei 15 mwaka huu wakati akizungumza na Viongozi, Wazazi, Walezi, Walimu na wanafunzi kwenye maadhimisho ya siku ya Familia duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mwere iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Fatma Mwassa amebainisha mambo mbalimbali ambayo yanapelekea mmomonyoko wa maadili kwa watoto ikiwemo ukuaji wa teknolojia, changamoto za uchumi, kuvunjika kwa ndoa na mambo mengine yanayofanana na hayo.
“...walimu, wazazi tushirikiane kukabiliana na mabaladhuri wanaoharibu watoto...” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kutowafumbia macho wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili kwa watoto badala yake watoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la TAG amewataka wazazi kutowaonea haya ndugu zao ambao wanafanya vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kuhofia kutengwa na ndugu hao.
Wakihojiwa kwa nyakati tofauti wanafunzi waliohudhuria maadhimisho hayo akiwemo Jane John anayesoma kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Morogoro ameeleza madhara ya vitendo vya ukatili kwa watoto na kutoa ushauri kwa wazazi na walezi kuongeza umakini juu yao ili kuwaepusha na vitendo hivyo vya kikatili.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.