Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amesema wazazi wote ambao hawajawapeleka shule watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, darasa la kwanza pamoja na awali watachukuliwa hatua kali za kisheria kwani kufanya hivyo wanawanyima watoto haki ya kupata elimu.
Fatma Mwassa ametoa tamko hilo Januari 23 mwaka huu wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kilichofanyika katika hoteli ya Morena iliyopo katika Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi Mhe. Fatma Mwassa amesema Serikali ya Awamu ya sita imetoa fedha za kujenga shule mapya, madarasa mapya, ununuzi wa madawati pamoja na kutekeleza sera ya elimu bila malipo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita.
Aidha, ameongeza kuwa pamoja na ukamilishaji wa madarasa kwa asilimia 100 na uwekaji wa madawati lakini mpaka sasa wanafunzi walioripoti shuleni kwa kidato cha kwanza ni asilimia 45 huku idadi kubwa ya watoto ambao walitakiwa kuwepo shule bado wapo majumbani na wazazi kutoa visingizio kuwa hawana fedha za kununulia sare za shule kwa watoto hao.
“...tunaomba watoto wote wanaotakiwa kwenda kidato cha kwanza waende shuleni vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mzazi...” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Viongozi katika Mkoa huo wamejipanga na watafanya msako nyumba kwa nyumba kwa lengo la kukagua watoto ambao bado wapo majumbani wakati walitakiwa kuwepo shuleni.
Katika hatua nyingine, Mhe. Fatma Mwassa amesema kuna haja ya kuwahamasisha wazazi kupitia kamati za shule kwa lengo la kuwapatia chakula cha mchana watoto wao pindi wawapo shuleni ili kuongeza ufaulu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando amesema amejipanga kufanya ziara ya kwenda kutembelea shule zote zilizopo katika Wilaya hiyo ili kubaini watoto wangapi hawajaripoti shuleni na kujua sababu inayosababisha hadi sasa wanafunzi hao kutoripoti shuleni na kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanaripoti katika shule walizopangiwa.
Aidha, Mhe. Albert Msando ameziagiza shule zote katika Wilaya hiyo kufanya tathmini ya idadi ya wanafunzi walioripoti katika shule zao kuanzia tarehe ya kufunguliwa kwa shule na ifikapo mwishoni mwa mwezi huu tathmini hiyo iwasilishwe kwake ili kubaini idadi ya wanafunzi ambao bado hawajaripoti shule.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewaelekeza watendaji wa ngazi zote katika Mkoa huo kubuni miradi ambayo itakuwa na manufaa na tija katika Mkoa huo ili kuyafikia malengo ya Mkoa kama walivyojiwekea.
Kikao kazi hicho kimelenga kutathmini hali iliyofikiwa katika Mkoa huo kimaendeleo na kubaini maeneo yenye changamoto na kwenda kuyafanyia kazi ili kuuboresha Mkoa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.