Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (Mb) amepiga marufuku ukodishaji wa mashamba kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa huku akiagiza uongozi wa Halmashauri na Wilaya hiyo kuacha kuwakodishia mashamba wananchi badala yake waweke utaratibu wa kuwagawia mashamba hayo Kwa mfumo wa ‘block farms’ ili wananchi hao waweze kukuza uchumi wao.
Waziri Bashe ametoa agizo hilo Februari 4 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mvumi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua skimu za umwagiliaji pamoja na kusikiliza kero za wakulima.
Aidha, ziara ya Bashe ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo alilolitoa hivi karibuni wakati wa ziara yake Wilayani humo, likimtaka Waziri huyo kufanya ziara katika Mkoa huo hususan wilaya ya Kilosa.
Waziri Bashe amesema Serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefuta mashamba 67 yenye jumla ya ekari 2700 ambayo yalikuwa hayaendelezwi na wawekezaji na kuagiza mashamba hayo kugawanywa Kwa wananchi wa maeneo hayo.
Aidha, amesema Halmashauri hiyo imekuwa ikiwatoza wananchi shilingi 10,000 Kama Kodi ya mashamba na kupiga marufuku mfumo huo na kuwataka kuacha kupokea fedha hizo kutoka Kwa wananchi badala yake watumie mfumo wa Block farms.
".. ni marufuku Halmashauri kuwakodisha mashamba wananchi..wakulima wasikodishiwe mashamba yaliyofutwa hati na Rais Samia Suluhu Hassani...” Amesema Waziri Bashe.
Sambamba na hilo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa Bwana Kisena Mabuba Kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wataalamu wa ardhi kuyapima mashamba hayo na kuyagawa Kwa wananchi Kwa mfumo wa ‘block farms’ Kwa lengo la kuyaendeleza.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa kilimo amekiagiza Chama Cha Ushirika cha UWAWAKUDA cha Dakawa Wilayani Mvomero kulipa fedha kiasi cha shilingi milioni 62 kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ifikapo Februari 6 na kuwasilisha nakala za makusanyo ya Mfuko wa Maendeleo ya Ushirika kwa Mkuu wa Mkoa huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa shukrani kwa ujio wa Waziri huyo amemuomba kupatiwa wakaguzi kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina katika chama cha ushirika wa UWAWAKUDA ili kubaini viashiria vya ubadhirifu wa fedha za wakulima na wanachama wa Ushirika huo.
Akielezea changamoto zinazoikumba Skimu ya Wami – Luindo Bi. Maimuna Makukika Mhandisi umwagiliaji Wilaya ya Mvomero amesema Skimu hiyo ina mifereji michache ambayo inakidhi hekta 172 tu huku skimu hiyo ikiwa na jumla ya hekta 956, za umwagiliaji, hivyo wakulima wameomba kujengewa mifereji mingine ili kuongeza ufanisi katika kilimo hicho.
Aidha, ameongeza kuwa mafuliko hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi unaathiri uzalishaji wao kutokana na mashamba yao kujaa maji yanayotokana na mafuliko.
Waziri Bashe wakati wa ziara yake ametembelea Skimu za umwagiliaji za Wami – Luindo, mashamba ya chama cha Ushirika cha UWAWAKUDA, na Skimu ya Rudewa iliyopo Wilayani Kilosa na kufanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi wa maeneo hayo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.