Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) ameitaka Mikoa yote nchini na Halmashauri zake kufanya ukarabati wa miundombinu ikiwa ni pamoja na viwanja vya michezo ili viweze kutumika katika michuano ya michezo inayoshrikisha Wizara, Taasisi na Idara za Serikali – SHIMIWI ambayo hufanyika kila mwaka katika Mkoa uliochaguliwa.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Oktoba 2 mwaka huu wakati akihitimisha kilele cha michezo ya SHIMIWI iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akivalishwa Scarf na Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Zacharia kabla ya kuanza kutoa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo.
Amesema, Mikoa na Halmashauri zote nchini zinatakiwa kufanya ukarabati wa Miundombinu kama viwanja vya michezo ili michezo itakayoandaliwa na Wizara yake katika Mkoa husika isiwepo changamoto yoyote ya kukwamisha michezo hiyo kufanyika kwa kisingizio cha miundombinu mibovu.
Aidha, Waziri Bashungwa alitumia jukwaa hilo kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hasaan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kurejesha michezo ya SHIMIWI ambayo ilikuwa imesimamishwa kwa miaka mitano iliyopita.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja (kushoto) akipokea moja kati ya zawadi za vikombe walivyoshinda timu ya RAS MOROGORO.
Sambamba na hayo Waziri amemhakikishia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango kutekeleza agizo alilolitoa Oktoba 23 mwaka huu wakati akizindua mashindano hayo kutathmini Taasisi, Wizara na Idara za Serikali ambazo hazikushiriki michezo hiyo na kwamba taarifa ya tathmini hiyo itawasilishwa katika Ofisi yake mara tu itakapokamilika.
Kwa upande wa changamoto zilizojitokeza kwa wanamichezo juu ya sintofahamu kwa washiriki wa michezo hiyo, Mhe. Bashungwa ametoa onyo kwa Viongozi wa SHIMIWI kutenda haki, na kuratibu vema michezo hiyo ili iwe huru na haki na kwamba Wizara yake itahakikisha inasimamia suala hilo ili kuondoa manung’uniko miongoni mwa wachezaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameipongeza Serikali kwa kuruhusu mashindano hayo kufanyika katika Mkoa huo licha ya Mikoa mingi iliyopo hapa nchini lakini Mkoa wa Morogoro uliteuliwa kuwa Mwenyeji wa mashindano hayo.
Sambamba na hayo, Shigela amebainisha mafanikio yaliyotokana na michezo ya SHIMIWI kwa kipindi cha wiki mbili za mashindano hayo ambapo amesema wingi wa wachezaji walioshiriki michezo hiyo umechangia kukuza uchumi wa wafanyabiashara na maendeleo ya Mkoa na taifa kwa jumla.
‘’…Tunasema asanteni sana ndugu zangu kwa kuja katika Mkoa wa Morogoro , uwepo wenu na ushiriki wenu tunauthamini, tutauenzi na kuuweka kwenye kumbukumbu kama watu muhimu mliochangia maendeleo katika Mkoa wa Morogoro.…’’ amesema Shigela.
Naye Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Zacharia amemuomba Mhe. Bashungwa kwamba zoezi la kushiriki michezo kwa watumishi wa Umma litekelezwe kwa mujibu wa sheria kutokana na takwimu kuonesha kuwa ushiriki wa Watumishi hao katika mashindano kunawajengea Afya Imara, Nidhamu, urafiki kuongeza ushirikiano, na kudumisha demokrasia na ufanisi wa kazi mahala pa kazi.
Mashindano haya ya 35 ya SHIMIMI yalianza Oktoba 20 mwaka huu na kuzinduliwa rasmi Oktoba 23 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango yakihusisha timu 47 ambapo jumla ya wachezaji 1,830 walishiriki.
Baadhi ya wachezaji wa timu ya mpira wa miguu TAMISEMI ambao waliibuka kinara katika mpira huo.
Mashindano ya mwaka huu yamehitimishwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) Novemba 2, 2021 ambaye alikuwa mgeni rasmi na kufanikiwa kugawa zawadi kwa timu ambazo zimefanya vizuri.
Kaulimbiu ya michezo hiyo ya SHIMIWI ilikuwa Michezo huleta Afya na ufanisi mahala pa kazi, jihadhari na UVIKO 19 chukua hatua nenda kachanje.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.