Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameiagiza tume ya Ushindani ya wizara hiyo kufuatilia kinachosababisha bei ya saruji kupanda katika baadhi ya Mikoa hasa katika Mikoa ya Kagera na Mwanza ili waweze kutatua changamoto hiyo.
Waziri Kijaji ametoa maagizo hayo leo Septemba 15, 2023 wakati wa Mkutano wake na waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kutoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa bidhaa hapa Nchini.
Amesema anatambua kuwa kuna changamoto ya nishati ya mafuta inayosababisha kwa namna moja ama nyingine kupandisha bei ya bidhaa hiyo ya saruji, hata hivyo amebainisha kuwa sio kwa kiwango ambacho bidhaa hiyo inauzwa.
“Naomba niwaelekeze tume yetu ya ushindani sasa iweze kupita kwenye maeneo yote na hasa Mikoa yetu ya pembezoni wapite na kuona bei ya Saruji ikoje kwa sasa kipi kinachosababisha bei ya saruji kuwa juu zaidi kuliko mikoa mingine...” amesema Dkt. Kijaji.
Sambamba na hilo amewataka wananchi kuuza mazao ya ziada waliyoyapata mwaka huu na kubakiza kwa ajili ya chakula kitakachotosheleza msimu mzima ili kuepuka baadae kununua chakula hicho kwa bei kubwa zaidi kuliko bei ya sasa.
Aidha, amewatahadharisha wafanyabiashara kuhusu Makampuni yanayowalaghai wafanyabiashara na Wananchi kuwa yanatoa kiasi cha fedha kama sehemu ya gharama za kujisajili ili waweze kushiriki katika ziara za kibiashara nje ya nchi na kwamba hao ni matapeli.
“niwaombe Wafanyabiashara na wenye viwanda nchini tunapoyaona matangazo haya kabla ya kufanya chochote ni vyema ukajiridhisha kwa kupata taarifa za fursa hizi kutoka kwenye Mamlaka za Serikali ikiwemo Taasisi yetu ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade) ambao ndiyo Taasisi yenye Mamlaka kisheria ya kuratibu masuala yote yanayohusu Maonesho na misafara ya kibiashara iwe ndani au nje ya Nchi yetu”. amesema Dkt. Kijaji.
Mbali na hayo, Waziri ametoa rai kwa wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuendelea kuongeza jitihada za uzalishaji wa bidhaa wanazozizalisha kwa kuzingatia ubora unaohitajika sokoni na kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema kwa kutumia mfumo wa stakabadhi Ghalani utasaidia wananchi kutatua changamoto ya bei ya mazao kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuwalaghai wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya chini yakiwa bado shambani suala ambalo Mkuu wa Mkoa amekemea kuwa ni kumnyonya mkulima.
Kwa sababu hiyo Mkuu wa MKoa bado anatoa ushauri kwa wakulima kuendelea kutumia kuuza mazao yao kupitia mfumo huo wa Stakabadhi ghalani kwa kuwa ndio pekee utakaowanufaisha na kuwakomboa katika kilimo.
Awali, akimkaribisha Waziri kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima alimueleza Waziri juu ya hali ya viwanda vya sukari Mkoani humo kuwa kiwanda cha Kilombero kinachopanuliwa na kiwanda cha Mkulazi kinachojengwa, vyote vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai mwakani na kwamba vitakapoanza uzalishaji, kwa pamoja vitazalisha jumla ya tani 200,000 kwa mwaka.
Waziri Dkt. Kijaji amefanya mkutano huo na wanahabari ikiwa ni Utaratibu wa kawaida kwa Wizara hiyo unaofanyika kila mwezi tarehe 15 kwa lengo la kudhibiti bei za bidhaa na kutoa taarifa ya bei halisi za bidhaa kwa wananchi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.