Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo ameuagiza uongozi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuunda tume maalum ili kuchunguza thamani ya fedha iliyotumika katika ujenzi wa Mradi wa Skimu ya umwagiliaji ya Lukenge Wilayani Mvomero pamoja na kuchunguza maendeleo ya mradi huo na kuwasilisha kwake taarifa ya uchunguzi huo ndani ya mwezi mmoja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo akitoa maelekezo kwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuunda tume kuchunguza mradi wa Skimu ya Lukenge Juni 17 Mwaka huu.
Dtk. Suleiman Jaffo ametoa agizo hilo Juni 17 Mwaka huu wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayosimamiwa na wizara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Kata ya Mtibwa Kijiji cha Lukenge.
Dkt. Suleiman Jaffo ameonesha kutokuridhishwa na utekelezaji wa Mradi huo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya Kiikolojia Vijijini - EBARR.
Mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi 600Mil. ulikuwa unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji NIRC kwa utekelezaji huo ambapo umekuwa wa kusuasua tangu mwaka 2012 hadi sasa.
Mfereji wa Skimu ya Lukenge ambao bado haujakamilika ujenzi na uliotembelewa wakati wa ziara ya Dkt. Suleiman Jaffo Juni 17 mwaka huu.
Aidha, Dkt. Jaffo amesema, kusuasua kwa mradi huo kunawanyima wananchi zaidi 3000 wa kijijini Cha Lukenge kunufaika nao ambao wanajishughulisha na kilimo cha hekta zaidi ya 1000, ambapo tija kubwa ya mazao yao yanategemea ukamilishwaji wa mradi huo.
“Nimekuja kuangalia thamani ya fedha katika mradi huu, sijaridhishwa kabisa na utekelezaji wake na hivyo nielekeze kwa uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuunda tume maalum ili kuchunguza na kukagua maendeleo ya mradi huu kisha kuniletea taarifa ndani ya mwezi mmoja” ameagiza Dkt. Jaffo.
Katika hatua nyingine Dkt. Jaffo amekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa EBARR wa kilimo cha umwagiliaji uliogharimu zaidi Tsh. 68Mil. unaotekelezwa katika Kata ya Lubungo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Kijiji cha Mingo ambapo pamoja na mambo mengine amewaagiza wanaotekeleza mradi huo kukamilisha mradi huo kabla au ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Naye Mwenyekiti wa Skimu ya Lukenge Bw. Hashim Omary akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amebainisha changamoto zilizokwamisha mradi huo ikiwemo kutopatikana fedha kwa wakti hali inayopelekea kasi ya ujenzi wa mradi kuwa ndogo.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na mratibu wa mradi huo Bw. Mteri Baraka ameweka bayana kuwa uwajibikaji mdogo na ukosefu wa watumishi wa Tume ya Umwagiliaji Tanzania ni sababu nyingine ya kusuasua kwa mradi hadi sasa, hivyo kumuahidi Waziri Suleiman Jaffo kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa kwa ufanisi.
Afisa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Mteri Baraka akitoa maelezo mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Dkt. Suleiman Jaffo juu ya maendeleo ya mradi Skimu ya Umwagiliaji ya Lukenge.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.