Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (MB) amezindua shamba la hekari 4000 litakaloendelezwa kwa ajili ya malisho ya mifugo ili kuwa na mifugo yenye tija kwa wafugaji na taifa kwa jumla.
Mhe. Kijaji amezindua shamba hilo Wilayani Kilosa Kijiji cha Mbwade Januari 3, 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani humo huku akisisitiza wafugaji na wakulima kuishi kwa amani na kila upande kuheshimu kazi ya mwenzake.
“…Mkoa wa Morogoro ni maalum kwetu ambayo inatakiwa kuwa mfano ndani ya taifa letu..." amesema Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
Akifafanua zaidi, Waziri Kijaji amesema shamba hilo la malisho litakuwa la mfano hapa nchini ikiwa ni hatua madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita kufanya mapinduzi ya sekta ya mifugo kwa kufuga kisasa ili kuwa na mifugo bora ambayo mazao yake ya yataweza kupelekwa katika masoko ya nje na kujipatia kipato hivyo kuondoa umaskini.
Sambamba na hayo, Mhe. Ashatu amewataka wananchi wa Mbwade na wa maeneo yote ya Mkoa huo kulinda na kutunza mazingira hususan vyanzo vya maji ili kuwa na maji ya uhakika ili kukidhi mahitaji ya wananchi wote na mifugo.
Akiwa katika shamba la kustawisha malisho la Kijiji cha Mandela Kata ya Magole Wilayani humo akizindua upandaji wa malisho ya mifugo aina ya Jun cao na Rhodes amewataka wafugaji kila mmoja kuwa na shamba lake la malisho sambamba na visima vya maji kwa ajili ya mifugo yake ili kuepuka ufugaji wa kuhama hama unaosababisha migogoro na ndugu zao wakulima.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema uchangiaji wa pato la taifa hapa nchini katika Sekta ya Mifugo imekuwa ikichangia kwa 7% hivyo ameahidi ifikapo mwaka 2030 uchangiaji wa pato la Taifa katika Sekta hiyo ufikie 10%.
Akimkaribisha Waziri kuongea na wananchi wa Kijiji cha Mbwade, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuomba Waziri kupata mbegu za malisho na mbegu za mifugo hususan Ng’ombe ili kupata mifugo yenye ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, amewataka wafugaji kuwa na maeneo ya malisho kwani amesema kutokuwa na maeneo ya malisho ndio sababu kubwa ya uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo chanzo kikubwa ni wafugaji kulisha mashamba ya wakulima.
Naye, Chifu wa kabila la Wamasai Bw. Matayani Simanga amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafugaji huku mfugaji Nyakungu Magairo wa Kijiji cha Mandela Kata ya Magole Wilayani Kilosa ambaye ana shamba la malisho amewashauri wafugaji wenzake kuacha ufugaji wa kuhama hama badala yake wafuge kisasa kwa kumiliki mashamba ya malisho na visima vya maji.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.