Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewataka Makamishna wa Ardhi nchini kufanya upekuzi wa mashamba yaliyomilikishwa katika maeneo yao ili wasio yaendeleza wachukuliwe hatua za kubatilisha miliki zao kisha kupewa watu wengine.
Mhe. Lukuvi ametoa agizo hilo Juni 8, mwaka huu wakati wa ziara yake Wilayani humo iliyolenga kurejesha mashamba hayo kwa wananchi yaliyobatilishwa na Serikali baada ya kuona hayaendelezwi.
‘’Makamishna wa Ardhi wa Mikoa yote hakikisheni mnafanya upekuzi wa mashamba yote yaliyomilikishwa katika maeneo yenu ya Mikoa ili wale wasiyoyaendeleza hatua za kisheria zichukuliwe za kubatilisha miliki ili wapewe watu wengine’’ Amesema Mhe. Lukuvi.
Aidha, Mhe. Lukuvi amesema kuna mashamba mengi nchini ambayo hayaendelezwi hali ya kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi ambao wanahitajio la mashamba hayo kwa ajili kufanya shughuli mbalimbali za kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa jumla.
Sambamba na hayo, Mhe. Lukuvi ametoa miezi miwili kwa Maafisa Ardhi Wilayani Mvomero kufanya upekuzi wa mashamba 86 yaliyotelekezwa na wamiliki wake ili yawasilishwe kwenye mamlaka husika kwa lengo la kufutwa na kurejeshwa kwa wananchi.
‘’Nataka haya mashamba 86 ambayo tunaamini kwamba hayaendelezwi vizuri yafanyiwe upekuzi haraka ili tujue yale ambayo hayafanyiwi kazi vizuri tupeleke kwa mamlaka hatua zichukuliwe, yafutwe ili wananchi wengine wanaotaka kuendeleza Ardhi hiyo kwa faida waweze kuyaendeleza’’.
‘’Hatuwezi kuacha wananchi wanabanana hawana Ardhi ya kutumia lakini kuna watu wana mashamba 86 hapa yamepimwa hayalipiwi kodi ya Ardhi, hawayaendelezi halafu wanasababisha uvamizi’’ Amesema Mhe. Lukuvi
Pia, Mhe. Lukuvi amesema mashamba 9 yenye hekari 13, 900.5 yamefutwa katika Kijiji cha Wami Luhindo ambapo hekari 9, 700 kati hizo watapewa wananchi na 4,100 zinazobaki zitatengwa kwa ajili ya wawekezaji ambao watakuwa wanalipa kodi kupitia mashamba hayo, hali ambayo itasaidia kukua kwa uchumi katika Wilaya hiyo..
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela, amewataka wanachi na watendaji wa Serikali Wilayani humo kutekeleza maagizo ya Mhe.Waziri Lukuvi ili migogoro ya Ardhi iweze kupungua ama kuisha kabisa katika Wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Shigela amewataka watendaji ngazi ya Vijiji kuzingatia sheria ya umiliki wa Ardhi na sheria ya kupanga matumizi ya Ardhi kwa lengo la kutokuwa chanzo cha migogoro kwa wananchi wanapohitaji Ardhi kwa ajili ya matumizi ya shughuli za maendeleo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.