Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mnyaa Mbarawa amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za Ujenzi wa Reli ya kisasa ya Mwendo kasi – SGR ambayo inatarajia kuanza safari zake Mwezi Julai mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kulia) baada ya kuwasili na treni ya umeme kutokea Dar Es Salaam hadi Morogoro.
Prof. Mbarawa amesema hayo akiwa Mkoani Morogoro leo Machi 18, 2024 wakati wa majaribio ya awamu ya pili ya Reli hiyo ya mwendo kasi kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro na kurudi Dar es Salaam ikiwa na mabehewa 14.
Amesema, Reli hiyo ni matunda ya Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anafanya kila jitihada ya kupata fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Reli ya Mwendo kasi ambayo ameagiza ianze kufanya kazi ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
“yote haya yamekuja kwa sababu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na leo tunaona matunda yake” amesema Prof. Makame Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu wa MKoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kituo cha Kilosa cha reli hiyo ya mwendo kasi kitakuwa kiungo kikubwa kwa Uchumi wa Utalii ambapo amebainisha kuwa watalii wengi wanaokwenda Mbuga ya Wanyama ya Mikumi na Hifadhi ya Milima ya Udzungwa watakuwa wanashukia katika kituo hicho cha Kilosa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima (kulia) akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa (kushoto)
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakazi wa Mkoa huo na watanzania wote kwa jumla kuchangamkia fursa hiyo ya kutumia Reli ya mwendo kasi ambayo itasaidia kuwafikisha salama na haraka kutoka Morogoro Kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine wanayotaka Kwenda.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kuangalia uwezekano wa kujenga miundo mbinu iliyo bora ya Barabara ya kuzunguka kituo cha Reli ya mwendo kasi cha Mjini Morogoro ili miundombinu hiyo ifanane na uwekezaji mkubwa alioufanywa na Mhe. Rais kwa kujenga kituo hicho Pamoja na eneo la kuhifadhia mizigo (Contener Terminar).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa amesema Ujenzi wa Reli ya mwendo kasi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 98.98 kazi kubwa iliyobakia ni ujenzi wa reli hiyo kuingia bandarini huku akibainisha kuwa ujenzi wa kipande cha Morogoro hadi Makutupora ya Singida umefikia asilimia 96.7.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.