Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ifakara Mji Bi. Zahara Muhidin Michuzi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Afya TAMISEMI kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Ifakara ifikapo Mwezi Agosti mwaka huu.
Waziri Mchengerwa ametoa agizo hilo leo Mei 20, 2024 ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea miradi ya Maendeleo Mkoani Morogoro katika halmashauri za Ifakara Mji, Halmashauri ya Mlimba, Malinyi na Halmashauri ya Ulanga.
Amesema, hospitali hiyo inayojengwa kata ya kibelege imeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na mivutano ya kisiasa, hivyo ametoa maagizo kuwa ifikapo Agosti Mosi, 2024 hospitali hiyo iwe imekamilika na wananchi wake kuanza kupata huduma za Afya.
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji nchi nzima kuacha mivutano na Wanasiasa na kusababisha ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo, itampasa kuwachukulia hatua watendaji hao waliohusika ikiwa ni pamoja na kuwashusha madaraka yao.
Aidha, amesema, kwenye mivutano ya kisiasa wakiwemo Madiwani na kusababisha miradi mbalimbali ya maendeleo kusimama na kutokamilika kwa wakati atachukua hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kusimamisha Baraza la Madiwani husika.
"...mnapovutana Wanasiasa na watendaji, watendaji wanashindwa kufanya maamuzi mnawanyima haki wananchi kupata huduma sasa tarehe 1/8/2024 nataka kuja kuzindua jengo hili..".ameagiza Waziri Mchengerwa.
Sambamba na maagizo hayo, amemtaka pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mhe. Kassim Faya Nakapala kuhakikisha anasimamia na kuondoa mvutano uliopo baina ya Madiwani na hospitali hiyo kukamilika kwa kipindi alichotoa, lengo ni kutowakosea haki wananchi wa Ifakara kwa kukosa huduma za matibabu ambayo ni haki yao ya msingi.
Awali, akimkaribisha Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima alimuomba Waziri Mchengerwa kumaliza Mgogoro uliopo wa kutokamilika kwa Hospitali hiyo ambayo Serikali imetoa fedha shilingi Bil. 1.5 lakini ujenzi huo umeshindwa kukamilika kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita na wananchi kuwanyima haki yao ya kupata matibabu kwenye hospitali hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.