Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ruaha baada ya ujenzi wa kituo hicho kutokamilika kwa wakati.
Mhe. Mchengerwa ametoa agiza hilo Mei 22, 2024 baada ya kuanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo akianza na kukagua Kituo cha Afya cha Ruaha na kuonekana uamuzi wa ujenzi wa kituo hicho ni wa muda mrefu kilichokosekana ni nia thabiti ya kukikamilisha kwa wakati.
Amesema, mradi huo uliibuliwa na wananchi tangu mwaka 2019 hadi sasa pasipo kukamilika pamoja na jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kuhakikisha mradi huo unakamilika lakini kumekuwa na vikwazo vinavyosababisha wananchi kukosa huduma ya Afya ambayo ni haki yao ya msingi.
Kwa sababu hiyo Waziri Mchengerwa hakuridhishwa na kasi ya ujenzi huo na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ulanga Bi. Saida Mahugu pamoja na timu yake kukamilisha ujenzi huo ifikapo Juni 30 mwaka huu bila kuwa na nyongeza ya muda mwingine
".... ninawataka Kila mmoja wenu kufanya kazi usiku na mchana Kituo hiki kimalizike tarehe 30 mwezi wa sita hakuna nyongeza..."
Sambamba na maagizo hayo ametumia fursa hiyo kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Salim Hashim kwa kutoa fedha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Afya cha Ruaha ili kuhakikisha wapiga kura wake wanaondokana na usumbufu wa kufuata huduma ya Afya umbali mrefu.
Baada ya kutoa maagizo hayo Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye ni Waziri wa TAMISEMI alitembelea daraja la mto Luhombelo lililoharibiwa vibaya na mvua kubwa zilizonyesha kipindi cha karibuni daraja linalounganisha Kijiji cha Mwaya na Kijiji cha Mbuga Wilayani Ulanga na kutoa pole kwa wananchi wa vijiji hivyo kutokana na adha kubwa wanayoipata.
Hata hivyo, akiwa katika eneo la tukio, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kutoa kiasi cha fedha cha shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la muda kuwawezesha wananchi kupita na kupitisha mazao na bidhaa nyingine wakati wakisubiri ujenzi wa daraja la kudumu.
Awali akimkaribisha Waziri huyo wa TAMISEMI, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuwa maelekezo yote aliyoyatoa Waziri atayasimamia sambamba na kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi waweze kuanza kupata huduma ya afya.
Tayari Waziri huyo amekwishatembelea Halmashauri tatu kati ya Halmashauri Nne alizokusudia kuzitembelea ambazo ni Halmashauri ya Ifakara Mji, Halmashauri ya Mlimba, Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi na Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.