Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum) Mhe. George Mkuchika amewataka wazazi na walezi hapa nchini kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni ili kuweza kujua changamoto zinazowakabili na kuzitatua ili kuweza kuongeza ufaulu mashuleni.
Waziri huyo amesema hayo Oktoba 26, 2024 wakati akikagua ujenzi wa bweni na kuzindua madarasa mapya katika shule ya Sekondari Kingolwira iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa huo.
Aidha, Mhe. Mkuchika amesema ni wajibu wa wazazi na walezi kushirikiana na kamati za elimu za shule za Msingi na Sekondari kuhakikisha wanafuatilia watoto wao pindi wanapokuwa shuleni ili kuweza kuwasahihisha pale wanapokosea na kuweza kuongeza ufaulu wao mashuleni.
"..Wazazi wenzangu hakikisheni mnafuatilia maendeleo ya watoto wenu mashuleni.." amesisitiza Mhe. George Mkuchika
Pia Mhe. Mkuchika amewapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kuufanya Mkoa kuwa namba 3 katika uandikishaji hivyo amewataka wananchi hao kufanya kampeni za kistaarabu.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuchika amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka jitihada kubwa katika kuhakikisha changamoto katika Sekta ya Elimu zinaepukika hapa nchini na kuwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kutumia mapato ya ndani kujenga na kusimamia miradi na kuwaletea wananchi maendeleo.
Sambamba na hayo, Mhe. Mkuchika amesema hakuna nchi inayoendelea bila kuwepo kwa amani na upendo hivyo ni jukumu la kila Raia wa Tanzania kuhakikisha wanatunza amani na upendo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu ya nane choo pia ujenzi wa bweni shule ya Sekondari Kingolwira ambapo wanatarajia kuanzisha kitado cha tano na sita katika shule hiyo na kwenda kuondoa changamoto ya uhaba wa shule za (Advance level) katika Halmashauri hiyo.
Naye Bi. Shangwe Mose Mkuu wa Shule ya Sekondari Kingolwira amesema ujenzi wa madarasa 4 na matundu 8 ya vyoo umeanza Aprili 15, 2024 na kukamilika Agosti 8, 2024 ambapo mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 102 na laki nne pamoja na matengenezo ya viti na meza160.
Mhe. Mkuchika amezindua madarasa manne na matundu nane ya vyoo shule ya Sekondari Kingolwira, ametembelea ujenzi wa bweni la wanafunzi shule ya Sekondari Kingolwira, ametembelea ujenzi wa barabara ya (TACTIC) amekagua ujenzi wa Hopsitali ya Wilaya na kuzindua zahanati ya Mji Mpya ambapo miradi hiyo ipo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.