Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) ameutaka uongozi wa Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wadau na kutoa elimu kuhusu utendaji kazi wake ili wananchi waweze kuhamasika kuitumia na kukuza Uchumi wao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo hilo Julai 9, 2024 wakati akifungua Tawi la Benki ya PBZ Mkoani Morogoro hafla iliyofanyika katika eneo la Mtaa wa Nunge katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema, pamoja na uzinduzi uliofanyika leo, bado Menejimenti ya Benki hiyo ina wajibu wa kutoa elimu ya kutosha kwa wadau ili kujua zaidi masharti ya mikopo ya Benki hiyo hususan riba na masharti ya Benki hiyo.
“Toeni Elimu kwa wadau hasa kuhusu usimamizi wa mikopo hiyo na ufafanuzi kuhusu Riba” amesisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu ameitaka benki hiyo kutoa ufafanuzi kuhusu urejeshaji wa mikopo wanayokopa wananchi na lengo kuu liwe ni kuwasaidia wananchi kupata maslahi kupitia mikopo wanayoikopa na si vinginevyo.
Kwa upande wa wananchi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kufunguliwa kwa Tawi la benki hiyo Mkoani Morogoro inasogeza fursa kwa wananchi kuingia kwenye ujasiliamali kwa kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji lakini amewataka kuzingatia masharti ya mikopo wanayokopa ikiwemo sharti kurejesha fedha walizokopa kwa wakati.
Hata hivyo Waziri Mkuu amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri wa kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi kupitia taasisi za kifedha na kurahisisha kuifikia huduma hiyo kwa njia ya mitandao na njia nyingine.
Amesema, Taasisi za kifedha ndizo zinazochagiza kukua kwa Uchumi hapa nchini zikiwemo Benki mbalinbali Pamoja na benki ya PBZ, hivyo amewataka wananchi kuchangamkia kufunguliwa Tawi la PBZ kama fursa kwao ya kukuza uchumi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Waziri wa fedha Zanzibar, amesema Benki ya PBZ itawasaidia wakulima mbalimbali katika shughuli zao za kilimo wakiwemo wakulima wa Mpunga wanaoishi Zanzibar na kufanya shughuli zao za Kilimo Mkoani Morogoro.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameupongeza uongozi wa Benki ya PBZ kwa uamuzi wao wa kufungua tawi lao Mkoani humo na kwamba uamuzi huo ni wa muhimu kwao na kwa Mkoa huo kwa kuwa Morogoro ndio Mkoa wa kilimo wa mazao mbalimbali ikiwemo zao la Mpunga, Miwa, mahindi, Ndizi, mazao ya Viungo na mazao mengine hivyo, benki hiyo itahamasisha Uchumi wa kilimo ndani ya Mkoa huo ikisaidiana na ujio wa Reli ya mwendo kasi ya SGR.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Bw. Arafat Haji ameelezea mafanikio ya Benki hiyo kuwa ni benki ya saba kwa ukubwa hapa nchini ambayo hadi sasa imewekeza rasilimali yenye thamani ya Tsh. Trilioni 2.2.Benki ya PBZ ilianzishwa Mwaka 1966 Visiwani Zanzibar ikiwa ni Benki ya Watu wa Zanzibar kwa sasa imeenea katika mikoa mingi hapa nchini ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara na sasa Morogoro huku wakitarajia kufungua tawi jingine Mkoani Mbeya.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.