Kufuatia agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa Disemba 22 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa ujazaji maji katika Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameitisha kikao cha kujadili viongozi mbalimbali wa serikali na wa kisiasa ili kujadili na kuweka mikakati ya kudhibiti uharibifu wa Mazingira na vyanzo vya maji Mkoani humo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha pamoja na Mawaziri wa Kisekta, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Viongozi wa Mkoa na Wilaya, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na wilaya za Morogoro kujadili changamoto za usimamizi wa ardhi ndani ya mkoa huo kwenye ukumbi wa Magadu katika Manispaa ya Morogoro, Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) na kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Angela Kairuki (Mb).
Viongozi mbalimbali wa ngazi ya Wilaya, Mkoa na hata Wizara wakiongozwa na Waziri Mkuu, wamekutana katika kikao kazi hicho kilichofanyika Disemba 24 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano Magadu Mesi mjini Morogoro lengo kuu ni kujadili changamoto za utunzaji wa mazingira, vyanzo vya maji na changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo ambauo ndiyo Sekta inayotoa fursa kubwa za uchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati anafungua kikao hicho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa 11 yenye changamoto ya uwepo wa mifugo mingi na migogoro mingi hapa nchini ikifuatiwa na mikoa ya Tanga, Iringa, Rukwa, Katavi, Tabora, Lindi, Arusha, Kigoma na Manyara.
Mikoa hiyo imekuwa na changamoto ya kutokuwa na usimamizi mzuri katika sekta ya mifugo na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi na ya wakulima na wafugaji.
Aidha, Mhe. Kassim Majaliwa amesema changamoto hizo za mifugo mingi kuliko uwezo wa maeneo zina athiri mfereji unaopeleka maji katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambalo linategemewa kuzalisha umeme wa Megawati 2115.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kutokana na changamoto za mifugo kumeibuka tabia za ukatili ikiwemo mauaji, uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira, uharibifu wa mazao ya chakula pamoja na uharibifu wa hifadhi za misitu iliyohifadhiwa kisheria.
Sambamba na hilo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewataka viongozi kusimamia sheria, kanuni na taratibu ambazo nchi imejiwekea katika kutekeleza wajibu hivyo ni jukumu lao viongozi kila mmoja kwa nafasi yake kutambua nafasi yake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mhe. Lucas Lemomo amesema wao kama wawakilishi wa wananchi wameyapokea maelekezo yote ambayo Waziri Mkuu ameyatoa ya kuhakikisha kuwa maeneo yote yenye vyanzo vya maji yanalindwa, kutumia busara kwenye kutatua changamoto ya mifugo katika maeneo ya mabonde na kilimo na kutoa elimu kwa wananchi katika kila eneo kuhusu uvunajinmifugo.
Awali wakati akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amemshukuru Mhe. Kassim Majaliwa kwa ujio wake na kumthibitishia kuwa viongozi na wananchi katika Mkoa huo wapo tayari kupokea maelekezo ya utekelezaji ambayo Waziri Mkuu atayatoa katika kikao hicho huku akigusia namna Mkoa ukivyojipanga katika kulinda vyanzo vya maji kwa kuwaondosha wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo lakini pia mkoa ulivyojipanga katika kuboresha sekta ya mifugo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.