Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo cha reli ya kisasa ya Mwendokasi - SGR kilichopo Kihonda katika Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Kassim Majaliwa amesema hayo leo Septemba 12 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es salaam hadi Kilosa Mkoani morogoro.
Amesema hadi sasa maendeleo ya ujenzi wa reli hiyo yanaridhisha kwa asilimia 99 hivyo wanatarajia kituo hicho kuanza kufanya kazi kati ya Disemba mwaka huu na Januari mwaka ujao.
‘’Tumeridhishwa na kazi inaendelea vizuri, na tukiwa tunaendelea na ukaguzi huu ni lazima tuipongeze Wizara ya Ujenzi pamoja na Shirika lenyewe TRC’’ amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe. Kassim Majaliwa amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela kwa kuweka mikakati mizuri ya ujenzi wa kituo cha mabasi katika stendi hiyo ya SGR kwa lengo la kuwarahisishia abiria safari za kwenda mikoani na kumtaka kuendelea kusimamia ujenzi wa stendi hiyo.
Sambamba na hayo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kutenga maeneo mahususi katika kituo cha reli ya mwendokasi kwa ajili ya Machinga ili kutowaruhusu kuzagaa katika maeneo ya kituo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema hadi sasa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeshatenga Shilingi Mil. 500 za ujenzi wa stendi hiyo ambayo itakuwa inahudumia abiria watakaofika katika stendi hiyo.
Pia, Shigela amesema stendi hiyo itapangwa maeneo ambayo yatawekezwa kwa ajili ya Hoteli pamoja na wafanyabiashara wadogo ili wananchi wa Mkoa huo wafaidike na uwepo wa SGR katika Mkoa wa Morogoro.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amesema amepoea maagizo ya Waziri Mkuu na kuahidi kusimamia ipasavyo maagizo hayo kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi zote za Mkoa huo.
Akizungumzia suala la ujenzi wa makazi karibu na mradi huo, Msando amesema Manispaa itasimamia vizuri mradi huo kwa kuzuia ujenzi holela katika maeneo ambayo mradi huo umepita kwa kuhakikisha majengo yanayojengwa yanafuata kanuni na taratibu ambazo zimewekwa na Manispaa ya Morogoro.
Bonyeza link hii hapa chini utazame tukio hilo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.