Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amekagua Kituo cha Reli ya Mwendokasi (SGR) kinachoendelea kujengwa Kihonda Mkoani Morogoro na kusema kuwa ameridhishwa na ujenzi huo.
Kauli hiyo ya kuridhishwa na ujenzi huo ameitoa Novemba 18 mwaka huu alipotembelea kituo hicho ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kwa mara ya pili na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Waziri Mkuu kwa awamu nyingine.
Mhe. Majaliwa amesema hayo mara baada ya kukagua Kituo hicho na kuwataka wakandarasi kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili kuwasaidia Watanzania kunufaika na uwepo wa Mradi huo.
“Mimi niwape taarifa, nimepita humu ndani nimeona kazi, nimeridhishwa na kasi ya Ujenzi huu, na sasa ndugu zetu wa Yapi Merkezi endeleeni kuchapa kazi kamilisheni mradi huu kwa muda ambao tumepangiana” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, amesema reli ya mwendokasi itakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia biashara mbalimbali zitakazoendeshwa katika kituo hicho ambapo wafanyabiashara watapata fursa ya kusafirisha bidhaa zao kwa muda wanaoutaka.
Pia, Mhe. Waziri Mkuu amesema reli hiyo ilitakiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu lakini kutokana na janga la CORONA ilisababisha ujenzi huo kusimama huku akiwahakikishia Wananchi kuwa hadi mwezi April 2021 reli hiyo itaanza kufanya kazi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri Mkuu ameagiza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Jeshi la Magereza Mkoani humo kuwasilisha Nyaraka walizo nazo katika Ofisi yake ambazo zinaonesha umiliki wa eneo la Kilimanjaro Sisal lililopo Kihonda katika Manispaa hiyo ifikapo Novemba 28 ili kutambua uhalali wa eneo hilo ambalo kwa sasa pande hizo mbili hazijakubaliana juu ya umiliki wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema uwepo wa Reli ya Mwendokasi katika Mkoa wa Morogoro utatoa fulsa kwa wafanyabiashara, Wajasiliamali wadogo, wakulima na Wadau wengine kufanya biashara zao katika kituo hicho cha reli na kujiingizia kipato na hivyo kukuza uchumi wao.
Akizungumzia hatua ya ujenzi wa reli hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, amesema pamoja na changamoto ya COVID – 19 kusababisha vifaa vya ujenzi huo kukwama kwenye nchi walikoagiza bado ujenzi wa kituo hicho umefikia zaidi ya asilimia 90.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema kituo cha reli cha mwendokasi – SGR kitakuwa ndio kitovu cha biashara Mkoani humo huku akitoa wito kwa wananchi wa Morogoro kujiandaa namna watakavyofaidika na kituo hicho kwa kuwa hata nchi zilizoendelea stesheni huwa ndio maeneo muhimu ya biashara.
Aidha, ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuweka uhusiano thabiti kati ya stesheni hiyo na maeneo mengine ya usafiri na usafirishaji kwa kuwa eneo hilo kwa sasa litakuwa mfano mahusus kwenye usafirishaji ndani ya Manispaa lakini pia kituo hicho kiwe dira ya Mji wa Morogoro kuelekea kuwa jiji.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.