Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha wanarudisha miundombinu ya Barabara kwenye maeneo ambayo miundombinu yake imeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Aprili 16 alipofanya ziara ya siku moja Wiliyani Kilombero Mkoani Morogoro Tarafa ya Mlimba kwa lengo la kutoa pole kwa wahanga wa mafuriko ya Mvua zinazoendelea kunyesha na zilizosababisha athari kubwa katika kata ya Masagati na Utengule Wilayani humo na kuamua kwenda kujionea mwenyewe hali halisi ya athari hizo.
Akiongea na wananchi wa Mlimba katika Mkutano wa hadhara, Waziri Mkuu amewataka watanzania kuendelea kuwa wavumilivu na kuridhia Serikali iendelee kushughulikia maeneo yenye changamoto kubwa na baada ya mvua kupungua ndipo serikali itafanya kazi ya kubwa ya kurudisha miundombinu hiyo ya barabara katika hali yake.
Aidha, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhi kutoa mbegu tani 189 za mpunga, mahindi na alizeti kwa ajili ya waathirika wa mafuriko hayo ili waendelee na shughulia zao za kilimo mara baada ya mafuriko hayo kuharibu mazao mashanbani mwao
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Kighoma Malima amemuomba Waziri Mkuu Tsh. 1 Bil. Kwa ajili kufanyia matengenezo reli ya TAZARA baada ya reli hiyo kuharib8wa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha na kuacha inaning’inia hivyo mawasiliano ya usafiri huo kukosekana tangu Aprili Mosi mwaka huu hivyo kusababisha adha kwa wananchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa kabla ya kumpokea Waziri Mkuu leo alikagua uharibifu wa Reli hiyo ya TAZARA na kujionea hali halisi ya uharibifu uliopo na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na kukata miti kandokando mwa Reli hiyo ili kuondokana na adha ya uharibifu wa Reli na kuleta adha kwao na hasara kwa taifa.
Kwa upande wa waathirika na mafuriko ya mvua wa kata ya Masagati na Utengule Wilayani Kilombero amemwambia Waziri Mkuu namna Mkoa ulivyojizatiti kuwasaidia waathirika hao chakula na mahitaji mengine huku akibainisha kuwa changamoto kubwa kutofikika kwa wananchi hao kwa kuwa wamezungukwa na maji hivyo akamuomba Waziri Mkuu usafiri wa Helikopta ili kuwapelekea chakula wananchi hao.
Kwa upande wake Regional Civil Eng. kutoka TAZARA Mhandisi James Mwasha amesema kwa tathmini iliyofanyika na kwa kasi iliyopo ya kurekebisha changamoto ya Reli hiyo kazi hiyo itakamilika ifikapo Aprili 28 mwaka huu na hasa kama watapata usaidizi wa kifedha.
Chakula ambacho kipo kwa ajili waathirika wa mafuriko hayo ya kata ya Masagati na Utengule ambcho hakijawafikia kwa sababu ya kutofikika ni Pamoja na Tani saba za mchele, kilo 350 za sukari, kilo 740 za maharagwe, lita 300 zamafuta ya kula na kilo 486 za chumvi
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.