Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na Madereva wa Serikali wakati akifungua Kongamanon la siku tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka madereva wa serikali kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kazi yao huku akibainisha kuwa madereva wana mchango mkubwa katika kutekeleza shughuli za serikali.
Mhe. Kassim Majaliwa amesema hayo wakati akifungua kongamano la siku tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Morena iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo madereva, kubadilishana uzoefu wa kazi sambamba na kujadili changamoto zinazowakabili.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa pamoja na viongozi mbalimbali akwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Mhandisi Masunga wakati wa kongamano la chama cha Madereva wa Serikali Tanzania.
"...ndugu washiriki mnatakiwa kuzingatia katika utendaji wenu wa kazi misingi na maadili ya utumishi wa umma, kuzingatia sheria za kazi na kuzingatia alama za barabarani..." amesema Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amesema kufanya kazi kwa kufuata taratibu, kanuni, maadili na kuzingatia alama za barabarani kutasaidia kupunguza na kudhibiti ajali za barabarani ambao ndio mpango mkakati wa serikali wa kudhibiti ajali hizo na kutaka madereva wa serikali kuwa mfano kwa madereva wengine.
Sambamba na hilo, Mhe. Majaliwa amewataka waajiri serikalini kutatua changamoto zinazowakabili madereva, kuimarisha uhusiano na kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima maeneo ya kazi, kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa kuwapa likizo madereva ili kupata muda wa kupumzika na hivyo kupunguza ajali zinazotokana na uchovu hivyo kuongeza ufanisi kazini.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na baadhi ya madereva wa Serikali baada ya ufunguzi wa kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka madereva hao kujiunga na mifuko ya pensheni ili baada ya kustaafu waweze kupata viinua mgongo na kusisitiza kuwa chama hicho ni muhimu kiwe na utaratibu unaofaa ili madereva wengi waweze kujiunga.
Kwa upande wake, Waziri wa ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) amesema Serikali imefanya maboresho ya muundo wa kiutendaji ambao hapo awali kulikuwa na changamoto ya kupanda madaraja ambayo tayari serikali imekwisha tatua sambamba na kuwabadilishia madaraja madereva waliokuwa na sifa.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Bashungwa amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za utumishi wa umma zimejipanga kuhakikisha Chuo cha Usafirishaji (NIT) kitaendelea kutoa mafunzo bora kwa madereva na maafisa usafirishaji na kwamba Wizara itashirikiana vema na chama hicho kutatua changamoto zinazowakabili Madereva wa Serikali.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima akitoa salamu za Mkoa amesema Serikali ya awamu ya sita imewafanyia mambo makubwa wananchi wa Morogoro na watanzania wote kwa jumla ikiwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya mwendo kasi, ujenzi wa kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo linatarajiwa kuzalisha umeme zaidi ya Megawati 2000 hivyo kutatua kabisa tatizo la umeme hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akitoa salam za Mkoa wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania.
Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) kiliazishwa Julai 7, 2013 na kusajiriwa mwaka 2015 kikiwa na malengo ya kuwaleta pamoja madereva wa Serikali, kutatua kwa pamoja changamoto zinazowakabili na kukemea matendo yanayoleta hasara kwa Serikali pamoja na kutetea Madereva kupata haki zao za kiutumishi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.