Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewataka Viongozi wa Serikali wa ngazi zote hapa nchini kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao hasa inayowagusa wananchi ili kuwaondolea kero zisizo za lazima.
Mhe. Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Julai 22, 2024 wakati wa Kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara, Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi za Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya na viongozi wa Chama Tawala wakiwemo Wenyeviti wa Mikoa na Makatibu wao kilichofanyika kwa njia ya mtandao kikiwa na lengo la kuwakumbusha viongozi hao kutekelza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo.
"... tunapaswa kusimamia utendaji wa utoaji huduma za jamii kusimamia shughuli ambazo wananchi wetu zinawagusa na kuzitumia kila siku kwa mfano Sekta ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Miundombinu ya barabara na Umeme ..." Amesema Mhe. Kassim Majaliwa
Kwa sababu hiyo, Waziri Mkuu amesisitiza Viongozi hao kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo, kuangalia iliyokwama na sababu zake na kisha kuitafutia majawabu na kuikamilisha kabla au ifikapo mwezi Disemba 2024.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Viongozi hao wa Mikoa kusimamia mila na desturi kwa jamii kwa kuwa na ajenda endelevu ya kuhakikisha vitendo viovu vinavyojitokeza sasa kutojitokeza hasa ulawiti, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa jamii ili kujenga nguvu kazi kwa Taifa la kesho.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Viongozi hao kusimamia na kulinda fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ili kusaidia baraza la madiwani kubuni na kuibua miradi muhimu ya maendeleo na kuzitumia katika miradi hiyo pasipo kutegemea fedha za Serikali kuu.
Sambamba na hilo, Waziri huyo amesisitiza Viongozi wa ngazi za Mikoa kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuwa na ajenda ya kudumu katika utekelezaji wake na kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na Umeme ili kuepuka matumizi ya mkaa na kuni ambayo ndio chanzo Cha uharibifu wa mazingira.
Sanjari na hayo, Waziri Mkuu amewataka Viongozi hao kutumia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo Tanzania itakuwa moja ya nchi mwenyeji wa AFCON 2027, kutumia mashindano hayo kutangaza vivutio vilivyopo hapa nchini ili kuwa na watalii wengi na kuongeza fedha za kigeni hapa nchini.
Hata hivyo, Mhe. Waziri Mkuu amewataka Kamati ya Ulinzi na Usalama kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii na kukanusha mara moja taarifa zisizo za kweli kila zinapojitokeza ili kuondoa taharuki ndani ya jamii zinazotokana na taarifa zisizo za kweli ili wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.
Sambamba na hilo, Mhe. Majaliwa amesisitiza juu ya umuhimu wa Viongozi wa Serikali na wale wa chama tawala kwa kila ngazi kuendeleza utamaduni wa kushirikiana katika kutekeleza ilani ya Chama kilichopo madarakani ili kuwa na uelewa wa pamoja hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa (MB) amesema maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kama yalivyokusudiwa kwa kuwa tayari ni maelekezo ya Serikali.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.