Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amewataka wafugaji nchini kufuga kwa tija ili kujipatia kipato na kujiepusha na migogoro baina ya wafugaji na wakulima hivyo kukuza uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.
Mhe. Mashimba Ndaki Waziri wa Mifugo na Uvuvi akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika maeneo ya machinjio ya Nguru Hills Wilayani Mvomero.
Waziri Ndaki ametoa wito huo Disemba 12 mwaka huu wakati wa Hafla ya uzinduzi wa machinjio ya kisasa ya nyama NGURU HILLS kilichopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
Mhe. Mashimba Ndaki amesema ni wakati sasa kwa wafugaji kubadilisha fikra zao na kuanza kufuga kisasa na ufugaji wenye tija kwao na ambao hauna athari kwa mazingira.
Mhe. Mashimba Ndaki akikagua mazingira ya eneo hilo la machinjio ya Nguru Hills.
Aidha, Waziri huyo amesema kufuga kama zamani kwa sasa hakuwapi maendeleo wafugaji hao, hata hivyo amesema kwa sasa dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la watu kwa hiyo ni lazima wafugaji wabadilike na kufuga kwa tija.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akikagua mazingira ya ndani ya machinjio hiyo ya kisasa ya Nguru Hills Wilayani Mvomero.
"Wito wangu wa mwisho ni kwa wafugaji lazima tubadilike fikra, kufuga kama ilivyokuwa juzi, jana na hata kesho kumeshapitwa na wakati, ndugu zangu nawaambia kila wakati kufuga kwa namna hiyo hatutaendelea....hatutaendelea hata kama mtakataa, kwenye kufuga kwa tija..." alisema Waziri Mashimba Ndaki.
Nyama ya Ng'ombe ambayo imehifadhiwa kisasa katika machinjio ya Ngulu Hills.
Sambamba na hilo Waziri Ndaki ametoa wito kwa wawekezaji wa kiwanda hicho kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa eneo linalowazunguka na watanzania kwa ujumla ambao wanasifa za kufanya kazi katika kiwanda hicho katika Sekta mbalimbali.
Aidha, amewataka pia kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozizalisha ili ziendane na soko la kimataifa, pia amewataka kudumisha mahusiano mazuri na wakazi wa maeneo hayo kwa lengo la kuepusha migogoro isiyo na lazima.
Muonekano wa miundombinu ya ndani ya machinjio ya Nguru Hills ikiwa katika hali ya usafi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akito tathmini ya hali ya mifugo katika Mkoa huo amesema Mkoa una jumla ya eneo la kilometa za mraba 73,039 ambazo ni sawa na hekta 7,303, 900, lakini eneo linalotumika kwa kilimo na ufugaji ni hekta 2,2269,396 na eneo la malisho ya mifugo ni hekta 394, 040.
Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa pamoja na viongozi wengine wakeweka jiwe la Msingi kuashiria ufunguzi wa Machinjio hiyo ya Kisasa.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa huo una Ng'ombe wa asili 1,126,883, mbuzi 468,210, kondoo 185, 487 na punda 9029.
Aidha, Mhe. Fatma Mwassa ameongeza kuwa Mkoa wa Morogoro una jumla ya Minada 35, Majosho 65 lakini yanayotumika ni 41, Marambo 42 na machinjio 9, Hospitali ya mifugo moja.
Aidha, Mhe. Fatma Mwassa amesema uzalishaji wa Ng'ombe kwa mwaka 2021/2022 ulikuwa tani 12,179 ambapo bei ya nyama ilikuwa shilingi 8,000 uzalishaji wa nyama ya mbuzi na kondoo ulikuwa tani 348. 6 huku nyama yao ikiuzwa kwa shilingi 10,000 kwa kilo.
Katika hatua nyingine Mhe. Fatma Mwassa amewataka wafugaji wa mkoa wa Morogoro kutumia vyema kiwanda hicho ambacho kimefunguliwa kwa kuvuna mifugo yao ili wabaki na mifugo michache, kujipatia pesa nyingi na kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa akitoa hotuba kwa Viongozi na Wananchi Wilayani Mvomero kwenye uzinduzi wa Machinjio ya Kisasa ya NGURU HILLS.
picha za pamoja za Mhe. Mashimba Ndaki Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa pamoja na viongozi wa CCM na Wawekezaji wa Machinjio ya NGURU HILLS.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.