Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wanasheria kutenda haki na usawa kwa watanzania wote katika kufanya kazi zao kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maono ya kuwa na jamii yenye haki, usawa, amani na maendeleo ili kujenga taifa lenye utulivu kwa maendeleo ya nchi.
Dkt.Ndumbaro amebainisha hayo Disemba 13, Mwaka huu wakati akizindua kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyofanyika katika eneo la stendi ya daladala ya zamani iliyopo Manispaa ya Morogoro kampeni ambayo baada ya uzinduzi huo itaendelea kufanyika katika Halmashauri zote 9 za Mkoa huo kwa siku 9 mfululizo ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria na kutatua kero zinazotokana na migogoro ya Ardhi, mirathi, Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Akifafanua zaidi Waziri huyo amesema "Mama Samia Legal Aid Campaign" imekwishafanyika kwa Mikoa 10 na Mkoa wa Morogoro ni wa 11 lengo ikiwa ni kuwafikia watanzania wote huku wataalamu wakutoa elimu hiyo na kutatua migogoro ya kisheria watafika katika kata 10 na vijiji 30 kwa kila Halmashuri za Mkoa huo.
Sambamba na hayo Waziri Ndumbaro amesema kampeni hiyo itaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu ndani ya jamii ikiwemo haki za wanawake na watoto, huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu wajibu na misingi ya utawala bora.
Aidha, kampeni hiyo itachangia kuboresha upatikanaji wa haki kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi pamoja na kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.
Katika hatua nyingine Waziri huyo amekemea vikali ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwani amesema huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kubainisha kuwa wanaojihusisha na vitendo hivyo wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani kwa waumini wao wayaishi maadili mema ili kulinda utamaduni kitanzania.
Hata hivyo. Mhe. Ndumbaro amewapongeza wananchi kwa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa na kupata Viongozi watakaoendana na 4R za falsafa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na kujenga taifa imara hivyo amewaasa kujiandaa na uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan kyobya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo una uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria kwani una changamoto nyingi zikiwemo Changamoto za ndoa, mgawanyo wa Mali na taraka.
Changamoto nyingine zinazojitokeza ndani ya Mkoa huo ni pamoja na Mirathi, Migogoro ya wakulima na wafugaji hususan Wilaya za mvomero, kilosa, Ifakara na maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro huku akiahidi Mkoa huo kutoa ushirikiano wote unaohitajika kwa Wizara ili kufanikisha kutatua kero za wananchi kupitia Kampeni hiyo.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.