Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa ameyaagiza makampuni ya mawasiliano ya simu hapa nchini kukamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano 758 inayoendelea kujengwa kote nchini kukamilika ujenzi huo kabla au ifikapo Mei 12 Mwaka huu.
Mhe. Silaa ametoa agizo hilo Machi 14, Mwaka huu alipotembelea kijiji cha Idete Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro ikiwa ni ziara yake ya kikazi ya siku moja Mkoani humo.
Akifafanua zaidi, Waziri Silaa amesema minara hiyo itawafikia watanzania zaidi ya Milioni 8.5 wa Mikoa tofauti tofauti huku Mkoa wa Morogoro ukiwa na minara 69 inayojengwa katika Kata 65 yenye Vijiji 169 katika Wilaya 7 za Mkoa huo, ambapo mpaka sasa minara 24 imekamilika na wananchi kuanza kutumia.
"Kupitia mradi wa ujenzi wa minara 758, jumla ya minara 69 itajengwa katika kata 65 yenye vijiji 169 vya Wilaya 7 za Mkoa wa Morogoro, ambapo mpaka sasa jumla ya minara
24 imekwisha washwa..." amesema Mhe. Jerry Silaa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema Wilaya ya Kilosa ina ujenzi wa minara 18 ambapo minara 9 kati yake imekamilika na kuanza kutumika na mnara wa Kijiji cha Idete unatarajiwa kukamilika Aprili 1 Mwaka huu.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema ujenzi wa mnara wa kidete umetoa ajira kwa vijana wa kijiji hicho kwa kushiriki ujenzi huo huku akiwataka wananchi kuendelea kuitunza na kuwa walinzi wa miradi hiyo inayojengwa ambayo Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa ajili yao.
Nao wananchi wa Kijiji cha Idete akiwemo Bi. Happiness Mkilani ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuwajengea minara ya simu itakayowasaidia katika mawasiliano changamoto ambayo imewasumbua kwa muda mrefu Kijijini hapo.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.