Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa (MB) ametatua mgogoro wa Ardhi wa muda mrefu baada ya wananchi wa Kata ya Mlabani kuvamia eneo lililokuwa linamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Ifakara tangu mwaka 1938 ambapo Kanisa limekubali kupewa fidia ya eneo jingine ili wananchi hao waendelee na shughuli zao katika eneo hilo.
Makubaliano hayo yamefikiwa Julai 8, mwaka huu baada ya Waziri Jerry Silaa kuwasili Wilayani Kilombero na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekali 500 ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara Mhashamu Salutaris Libena na kukubali kupewa fidia ya eneo jingine.
Awali wakati akifafanua kuhusu mgogoro huo, Waziri Silaa amesema wananchi ndio wa Kata ya Mlabani ndio waliovamia eneo hilo linalomilikiwa na Kanisa Katoliki tangu mwaka 1938. hivyo Kanisa hilo linahitaji fidia ya kupewa eneo mbadala ili kulitumia katika shughuli zake mbalimbali zikiwemo ujenzi wa vyuo, hospitali na huduma nyingine za wananchi.
“…nimefika hapa Wilayani kwenu mahususi kwa ajili ya mgogoro wa Mlabani… nimekuja kwa ajili ya kumalizia makubaliano ambayo Mhasham Baba Askofu Libena kwa busara zake amekubali kupewa eneo jingine …” amesema Waziri Silaa.
Kwa sababu hiyo, Waziri Silaa ametoa siku 90 kwa viongozi wa Serikali na wataalamu kutumia ramani husika ili kupima na kupanga eneo na baada ya kukamilika upimaji huo wananchi watalipia Tsh. 500 kwa mita moja ya mraba ili kupata hati ya eneo na kuwamilikisha ili kupata fedha za kununua eneo lingine la Kanisa hilo.
PiaMhe. Jerry amewataka wananchi kutunza hati zao amesema za umiliki wa ardhi kwani ndio kielelezo cha juu cha umiliki ili kuacha kutapeliwa ardhi na kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Dominic Kyobya amesema Wilaya hiyo ina maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi yakiwemo Mlabani, Kambenga, Rubada huku akifafanua kuwa eneo hilo ala Mlabani mbalo linamilikiwa na Kanisa Katoliki la Ifakara lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 500.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mhe. Abubakar Asenga amekiri kuwa eneo hilo ni la Kanisa ndio maana serikali imeshindwa kujenga shule, hospitali na vituo vya afya hivyo baada ya umiliki wa eneo hilo serikali itaweka utaratibu mzuri na kupanga mitaa ili kupata maeneo ya kujenga shule na kituo cha Afya.
Nao wananchi akiwemo Thomas Mwakilema Mkazi wa Mlabani amefurahishwa na ujio wa Waziri huyo na kukiri kuwa eneo hilo ni la Kanisa na kuahidi kutoa ushirikiano kutosha katika kulipia ili kupata hati ya umiliki na ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake hususan kwa kutatua changamoto hiyo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.