Waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameelekeza Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) kuwachukulia hatua kali za kisheria wavuvi haramu wanaofanya kazi hiyo bila kufuatia taratibu za uvuvi katika maeneo mbalimbali ya hapa nchini.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati wa mkutano na wavuvi.
Mhe. Ulega ametoa maagizo hayo Julai 5, 2023 wakati wa mkutano na wavuvi uliofanyika katika Kata ya Kivukoni iliyopo Halmashauri ya Mji Ifakara akiwa katika ziara yake ya siku mbili katika Wilaya za Kilosa na Kilombero Mkoani Morogoro.
Amesema, wavuvi haramu huvunja kanuni, taratibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa na wavuvi wote kwa kuharibu vyanzo vya maji na mazalia ya samaki, hivyo kupunguza uzalishaji na mapato kwa serikali.
"...wapo watu wanaofanya uharibifu katika vyanzo au mazalia ya wale samaki, wenyewe hayo mazalia mnayajua hivyo mnatakiwa kushirikiana na TAWA kudhibiti wavuvi haramu kwa manufaa mapana ya kwenu..."
Sambamba na hilo, Mhe. Ulega amesikitishwa na utitiri wa tozo unaowadidimiza wavuvi ikiwa ni pamoja na leseni 24000/=, kibali Tsh 15,000/=, kibali Cha siku Tsh 5000/=. Kwa sababu hiyo ameshauri kuwekwa gharama moja ili kuondoa kero ya malipo ya mara kwa mara kwani huo ni usumbufu kwa wananchi.
Kwa upande mwingine, Mhe. Ulega akizungumza katika mkutano huo wa hadhara amewataka wafugaji kutunza na kuthamini mifugo yao kwa kutafuta eneo maalum kwa ajili ya mifugo yao badala ya kulisha kwenye mashamba ya wakulima na kuiga mfano wa maisha ya wakulima wa kumiliki ardhi binafsi kwa ajili ya kilimo na kutaka wafugaji nao kumiliki ardhi binafsi kwa ajili ya malisho ya mifugo wao ili kuondoa migogoro baina ya jamii hizo mbili.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (kushoto) akiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega wakati wa mkutano na wavuvi.
Hata hivyo, Mhe. Ulega amesema wizara hiyo imejipanga kutoa hekta 10,000 eneo likilopo kata ya Mkata kwa ajili ya lunch itakayoitwa livestock guesthouse itakayochukua wafugaji wa muda mfupi ili kulisha mifugo yao huko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema uvuvi haramu ni ukiukwaji wa kanuni, taratibu na sheria za uvuvi na kuhatarisha usalama wa hifadhi pamoja na viumbe waliomo kwenye hifadhi hizo, hivyo ametoa wito kwa wavuvi hao kushirikiana na serikali kuwabaini waharifu hao Kwa maslahi mapana ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro na nchi nzima kwa jumla.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na wananchi wakati wa mkutano na wavuvi.
Naye, Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi nyanda za juu kusini TAWA Joas Makwati amesema kwa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania ya mwaka 2009 hairuhusu shughuli za uvuvi katika eneo lililohifadhiwa ikiwemo mapori tengefu ya Kilombero lakini kutokana na umuhimu na uhitaji wa wananchi na Halmashauri kutaka kupata mapato, Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2020/21 iliruhusu wananchi kuingia kwenye maeneo hayo na kuweka utaratibu Maalum, huku akiwataka wananchi kufuata kanuni na taratibu hizo.
Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi wa wanyama pori nyanda za juu kusini - TAWA Joas Makwati akizungumza na wananchi.
Nao wavuvi akiwemo Bw. Andrew Justine Mtolela ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi Cha wavuvi amesema wanafanya kazi hizo kiasili kwa kuunga na sera ya serikali ya utunzaji wa mazingira ili kuongeza uzalishaji na mapato katika Halmashauri hiyo huku akithibitisha kuwa kuna baadhi ya wavuvi wakitumia njia haramu ambapo ameahidi watashirikiana na TAWA na Serikali katika kuwabaini waharifu wote haramu.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.