Waziri Ummy atoa wiki tatu Majengo ya nyongeza kutoa huduma kwa wananchi
Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI Ummy Mwalimu ametoa wiki tatu kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro kuhakikisha majengo manne ya nyongeza yanayojengwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo yanakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Waziri Ummy Mwalimu ametoa agizo hilo leo Septemba 23 akiwa katika ziara yake ya siku moja Wilayani Mvomero ikiwa pia ni siku ya tatu tangu kuanza ziara yake Mkoani Morogoro na kutembelea ujenzi wa majengo hayo yanayojengwa kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya hospitali hiyo.
Baada ya kupata maelezo ya ujenzi huo, Waziri Ummy Mwalimu amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imeleta fedha kiasi cha shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo ya nyongeza.
Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu ametoa Wito kwa viongozi wa Halmashuri hiyo kutaka kazi ya ujenzi wa majengo hayo kukamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma za afya mapema na kuagiza kazi hiyo imekamilika mapema na ifikapo Oktoba 15 mwaka huu huduma za Afya kwa wananchi zianze kutolewa.
“kazi ni nzuri nimeridhika nayo ila ninachotaka ikamilike haraka, tunakubaliana tarehe 15 Oktoba Mheshimiwa hizo huduma zianze kutolewa hapa” aliagiza Waziri Ummy Mwalimu.
Pamoja na maelekezo hayo Waziri alionekana ameridhika na kazi nzuri iliyofanyika katika kujenga majengo hayo, hivyo kuahidi kuleta fedha nyingine kiasi cha shilingi 300Mil. kwa ajili ya kujenga majengo mengine ya kipaumbele zikiwemo nyumba za Watumishi wa Hospitali hiyo ikiwa ni fedha za bajeti ya 2021/2022 iliyoanza Julai mwaka huu.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy Mwalimu amesisitiza kuwa kila Halmashauri ijiwekee malengo ya kujenga miundombinu kwa kutumia fedha zinazotokana na makusanyo ya ndani kwa ajili ya kurudisha fadhila kwa wananchi kwa kuwajengea miradi ya maendeleo inayojielekeza kwenye huduma za kijamii kama maji, Zahanati, vituo vya Afya ama vyumba vya madarasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela yeye pamoja na kuishukuru Serikali kuleta fedha za kutosha kwa ajili ya miradi mbalimbali Mkoani humo ameiomba Serikali kuiangalia kwa jicho la kipekee Hospitali ya Wilaya ya Mvomero kwa kuwa hospitali hiyo iko kwenye barabara Kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mji wa Serikali Dodoma, hivyo kuna changamoto za ajali za mara kwa mara zinatokea eneo hilo na kuiomba serikali kuongeza Vifaa tiba na wataalamu kwa maana ya madaktari bingwa kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo inapotokea.
“ombi letu ni upatikanaji wa Wataalamu pamoja na vifaa ili hospitali yetu sasa iweze kufanya kazi inavyotakiwa hususan wakipatikana madaktari bingwa” amesisitiza Martine Shigela.
Mhe. Ummy Mwalimu amekamilisha ziara yake ya siku tatu Mkoani Morogoro kwa kutembelea shule ya Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine kwa kukagua ujenzi wa mabweni na Bwalo la chakula la wanafunzi yanayogharimu jumla ya shilingi 700 Mil. huku akionekana kutoridhishwa na matumizi ya fedha hizo na kuahidi kutuma timu ili kuhakiki matumizi sahihi ya fedha hizo.
Halmashauri nyingine alizotembelea Waziri Ummy Mwalimu katika ziara yake ya siku tatu Mkoani hapa ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.