Waziri wa Denmark asisitiza watanzania kutunza mazingira
Waziri wa Denmark anayeshughulikia Ushirikiano wa Maendeleo na Sera ya Hali ya Hewa Nchini humo Mhe. Dan Jorgensen ametaka watanzania kuendelea kutunza mazingira ili kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi (Climate change).
Mhe. Jorgensen ametoa nasaha hizo Aprili 4, 2024, alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro katika hifadhi ya milima ya Udzungwa pamoja na kutembelea shughuli nyingine za maendeleo.
Katika ziara hiyo ambayo aliambatana pia na Balozi wa Denmark hapa Nchini Mhe. Mette Stipend amesema ni vema watanzania wakaendeleza tabia ya kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na upandaji miti ili mazingira ya Tanzania yafanane na hali ya milima ya Hifadhi ya Udzungwa na kupongeza hali hiyo.
Katika hatuanyingine Waziri huyo ameonekana kufurahishwa na kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ajenda ya utunzaji wa mazingira pamoja na kuweka mazingira mazuri ya Utalii.
Moja ya shughuli za maendeleo alizozitembelea ambazo ziko Wilayani Kilombero ni pamoja na mradi wa nyuki wa kikundi cha Njokomoni cha Mang'ula kinachozalisha Asali na utunzaji wa Nyuki, Mradi wa njia ya Tembo (Step) na Kituo cha utafiti cha Udzungwa.
Pia Waziri huyo alitembelea Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na kupongeza uwekezaji wa Bilion 600 wa ujenzi wa kiwanda kipya (K4).
Aidha, alipata wasaa wa kutembelea Hifadhi ya Milima ya Udzungwa na kufurahishwa na mandhari ya milima hiyo na kuahidi kuwa atakuwa Balozi wa kuvutia watalii wa kutoka nchini kwao hapa Tanzania hususan kutembelea Hifadhi hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.