Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis amesema Wizara yake ipo tayari kushirikana na wataalam, wakulima na viongozi wa Mkoa wa Morogoro katika kuongeza uzalishaji wenye tija wa mazao ya kimkakati hususan zao la karafuu kwa lengo la kuinua uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.
Mhe. Shamata ameyasema hayo Agosti 3, 2023 alipotembelea banda la Halmashauri ya wilaya ya Morogoro ambayo inalima zao karafuu wakati alipotembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro.
Aidha, Mhe. Shamata Khamis amesema kutokana na umuhimu wa zao hilo katika kukuza kipato cha wakulima na taifa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya kilimo itashirikiana na Mkoa wa Morogoro kwa karibu zaidi na kuhakikisha mazao hayo yanakuwa na tija.
Kwa msingi huo, Wizara hiyo inatoa nafasi kwa wataalam na wakulima kutoka Mkoani Morogoro kwenda Zanzibar kupata elimu na ujuzi wa uzalishaji wa mazao hayo.
“...nitoe wito tuendelee kuungana, kushirikiana kubadilishana wataalam, kufanya vikao vya pamoja ili kuhakikisha mazao haya yanakuwa na tija ya uzalishaji..” amesema Mhe. Shamata Shaame Khamis.
Sambamba na hilo, Mhe. Shamata wakati akiwa kwenye banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesisitiza watendaji wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na kwa ushirikiano ili kutimiza lengo la serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemshukuru Waziri huyo kwa kutembelea maonesho hayo Kanda ya Mashariki na kukubali kupokea wataalam ambao watapata uzoefu juu ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati hususan zao la karafuu.
Mhe. Malima ameongeza kuwa itaundwa timu ya wataalam 30 wakiwemo wakulima 20, maafisa kilimo 5, waandishi wa habari 5 ambao wataenda kujifunza namna bora ya uzalishaji wa karafuu, aidha, amesema ziara ya Waziri huyo itafungua fursa za kilimo kwa wakulima wa Kanda ya Mashariki.
Kwa niaba ya waoneshaji, Bw. Abdalah Mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ambaye ana ulemavu wa macho amesema maonesho ya Nanenane 2023 hayajawaacha nyuma watu wenye ulemavu ambapo imetoa fursa kwao kuonesha ujuzi walionao, hivyo ameishukuru Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia nafasi hiyo. Ameongeza kuwa amebuni kifaa cha kuingiza uzi kwenye sindano kitakacho wasaidia mafundi wasioona kushona nguo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.