Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mhe. Kisena Mabuba ametoa wito kwa Maasifa Habari na Mawasiliano wa Serikali nchini kutimiza wajibu wao ili kutekeleza majukumu ya kuisemea Serikali.
Wito huo umetolewa Kilosa, Mkoani Morogoro wakati wa ziara ya Uongozi wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali pamoja na Idara ya Habari- MAELEZO walipotembelea Halmashauri hiyo kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Maafisa Habari.
Mhe. Mabuba amesema, kuna changamoto kwa baadhi ya Maafisa Habari katika kutekeleza wajibu wao na hii kupelekea wananchi kutokujua yanayofanywa na serikali yao.
“Nimekuwa mdau wa habari kwa miaka mingi, nimeishi na kuiheshimu taaluma hii ya habari, naamini Chama hiki kitatatua changamoto zinazoikabili taaluma hii ili kuweza kutimiza wajibu wa kuisemea serikali” amesisitiza Mhe. Mabuba.
Ameongeza kuwa, kwa miaka takribani minne aliyotumika kwenye nafasi aliyopo hakuwahi kuona Viongozi wa TAGCO wakitembelea vitengo vya habari, hivyo ujio huo utakuwa na manufaa katika ofisi mbalimbali za habari ndani ya Serikali.
Aidha, Mhe. Mabuba amefafanua kuwa, katika uongozi wake Ofisi ya Habari ataipa kipaumbele kwani kupitia Ofisi hiyo wananchi wanaelewa na kujua kile kinachotekelezwa na serikali katika Halmashauri yake.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Tendaji kutoka TAGCO Bw. Karimu Meshack amesisitiza kuwa, ni vyema Maafisa habari kutumia mbinu za kisasa kuwasiliana na wananchi katika maeneo yao kwa kutoa taarifa za miradi yote inayotekelezwa na ile inayoendelea kutekelezwa na serikali.
“Tutumie vyombo vyote tulivyonavyo kwa mfano, mitandao ya kijamii, blogs, website, magazeti na redio hasa za kijamii kwa kuwa wananchi wanahitaji kusikia yanayofanywa na serikali yao kwa maslahi mapana ya nchi” amefafanua Bw. Meshack.
Uongozi wa Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO), Mwakilishi Idara ya Habari - MAELEZO upo Mkoani Morogoro kwa lengo la Kufuatilia utendaji kazi wa maafisa habari katika Halmashauri za Mkoa huo, na kuweka mikakati ya pamoja katika kuimarisha mawasiliano baina ya Serikali na wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.