Vijana Mkoani Morogoro wametakiwa kujitokeza kwenye matamasha yanayoandaliwa kufanyika Mkoani humo lakini zaidi kupata Elimu ya Ufundi Stadi ili kuweza kujiajiri na hivyo kukuza uchumi wao, wa familia zao na Uchumi wa Taifa kwa jumla.
Wito huo umetolewa Agosti 23 mwaka huu na Meneja wa shirika la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Morogoro (MVIWAMORO) Bw. Samweli Makwatwa wakati wa kikao kazi cha kutambulisha Tamasha la Vijana linalotarajiwa kufanyika Mkoani humo mwezi Novemba mwaka huu.
Bw. Makwatwa amesema lengo la matamasha hayo ni kuwakutanisha vijana ambao wamepatiwa elimu ya ufundi stadi na kukuza ujuzi wao ili waweze kuonesha ujuzi huo kwa vijana wengine juu ya elimu waliyoipata ya ufundi stadi ili vijana wengine wahamasike na elimu hiyo.
Aidha, Meneja huyo ametoa wito kwa vijana kujikita katika kupata elimu ya ufundi stadi ambayo itawasaidia kujiajiri kuliko kutegemea ajira rasmi kutoka Serikalini.
Sambamba na hilo ameiomba Serikali kuwasaidia vijana kupata elimu hiyo kwa kuwa ndiyo njia pekee itakayowasidia kujikwamua kiuchumi kupitia kujiajiri.
Hawa ni baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye kikao.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa Mradi wa Opportunities for Youth Employment (OYE) Bi. Diana Meshy amesema mradi wa OYE umelenga kuwafikia Vijana 4,250 kutoka Mikoa ya Morogoro na Singida kwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia mafunzo mbalimbali ya kilimo, ufugani na uvuvi.
Afisa Mawasiliano wa Mradi wa Opportunities for Youth Employment (OYE) Bi. Diana Meshy akizungumza wakati wa kikao cha kutambulisha tamasha la vijana.
Matamasha hayo yatafanyika katika Halmashauri tano za Mkoa wa Morogoro ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Malinyi pamoja na matamasha hayo kufanyika ngazi ya Halmshauri pia kutakuwa na tamasha kubwa ngazi ya Mkoa ambalo litafanyika mwanzoni mwa Mwezi Novemba mwaka huu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.