Wito umetolewa kwa wafanyabiashara hapa nchini kusajili biashara zao ili kupata leseni za biashara hizo kwa lengo la kutambulika na Serikali na kupata taarifa sahihi mahali zilipo, kujua mwenendo wa biashara hizo na Serikali kuelekeza fedha zake kwa wafanyabiashara hao wanaotambulika rasmi.
Wito huo umetolewa Machi 20, 2024 na Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bi. Loi Mhando wakati wa maonesho ya ujasiliamali kwa wanajumuiya ya Chuo kikuu cha Mzumbe kilichopo Wilaya Mvomero Mkoani Morogoro kuelekea siku yao ya Mzumbe (Mzumbe Day) inayofanyika chuoni hapo kila mwaka.
Bi. Mhando akifafanua zaidi amesema, wafanyabiashara hawana budi kusajili biashara zao na kupata leseni za biashara wanazofanya, lakini pia kuwa na usajili wa alama za biashara na huduma na utoaji wa leseni za biashara na viwanda huku akibainisha kazi mbalimbali zinazofanywa na BRELA kuwa ni pamoja na kusajili makampuni.
“….Sisi tunatoa wito kwa wakazi wa Morogoro na viunga vyake kurasimisha biashara zao pia wafike Chuo kikuu cha Mzumbe watapata huduma zote zinazotolewa na BRELA” amesema Bi. Loi Mhando.
Katika hatua nyingine Bi. Mhando amesema lengo la kuwepo ndani ya siku tatu katika chuo Kikuu cha Mzumbe ni kutoa elimu kwa wanachuo na wahadhiri kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA hususan umuhimu wa kurasimisha biashara kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wao wanachuo wa chuo hicho cha mzumbe akiwemo Idi Mohamed amesema kuna urahisi wa kuanzisha biashara na kuirasimisha lengo ni kupata rasmi ulinzi wa kisheria na kumsaidia mfanyabiashara kuondokana na changamoto za kibiashara zinazoweza kujitokeza.
Maonesho hayo ya Ujasiliamali kuelekea Mzumbe Day yana lengo la kuhamasisha kazi za ujasiriamali kwa wanachuo na wahadhiri na yanafanyika kwa siku tatu kuanzia machi 20 hadi 23, 2024.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.