Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Mkoa wa Morogoro, inatarajiwa kuanza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa lengo la kusogeza karibu huduma hiyo ikiwemo utoaji wa Elimu inayohusu masuala ya haki na sheria na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Disemba 13, Mwaka huu katika eneo la stendi ya daladala ya zamani iliyopo Manispaa ya Morogoro na baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo itaendelea kufanyika katika Halmashauri zote za Mkoa huo kwa siku 10 mfululizo ikiwa na lengo la utoaji elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria kama vile Ardhi, Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mirathi, Ndoa, Ukatili wa Kijinsia, Madai, Jinai vilevile itahusisha huduma ya usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa na kifo vitakavyotolewa na RITA.
Ratiba iliyotolewa inaeleza kuwa, mara baada ya uzinduzi huo kampeni itaendelea kwenye ngazi ya Halmashauri ambapo itafanyika kwa kata 10 na vijiji 30 kwa kila Halmashauri ikigusa moja kwa moja kutatua changamoto za wananchi hususan masuala ya kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na utoaji wa Elimu ya haki za binadamu kwa ujumla.
Kampeni hiyo ya Mama Samia inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu ndani ya jamii ikiwemo haki za wanawake na watoto, huduma ya ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia pia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu wajibu na misingi ya utawala bora.
Kampeni hiyo inachangia uboreshaji na upatikanaji wa haki kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi pamoja na kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.
Ikumbukwe kuwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa Mikoa yenye migogoro lukuki inayohusu ardhi na migogoro mingine, hivyo, wananchi mnaombwa kushiriki kwenye kampeni hiyo na kushiriki kwa wingi ili wataalam waliopo kwenye kampeni hiyo waweze kutatua kero na migogoro inayowakabili.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.