Serikali Mkoani Morogoro imetoa zaidi ya Tsh. Bil. 12 kwa ajili ya vikundi 440 vya akinamama na kuhusisha wafanyabiashara 7411 waliosajiliwa ili kuwawezesha wanawake na wasichana kukuza uchumi wao na familia zao.
Hayo yamebainishwa Machi 8, Mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima maadhimisho ambayo kimkoa yamefanyika katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
"... Mkoa wa Morogoro umeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kina Mama..." amesema Mkuu huyo wa Wilaya
Aidha, Mhe. Kyobya amebainisha kuwa mkoani humo, wafanyabiashara wanawake waliothibitishwa ni zaidi ya 7,411, huku wafanyabiashara wanaume wakiwa 2,760. Takwimu hizi zinaonesha juhudi kubwa za wanawake katika kujitafutia riziki na kuchangia ustawi wa familia bora.
Katika hatua nyingine Wakili Dunstan Kyobya amesema, taasisi mbalimbali zinawajibu wa kutoa elimu ili kuepukana na matukio maovu ya ukatili wa kijinsia ikiwemo usagaji, ubakaji na ulawiti hivyo wanapaswa kuvikemea vitendo hivyo ili kutunza maadili katika jamii.
Kwa upande wao wanawake kupitia msoma risala wao Bi. Rosemary Ngonyani wamesema wanawake wameonesha umahili katika kuchukua mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3, kupitia mfuko wa 10% ya mapato ya Halmashauri na mikopo mingine inayolenga kuimarisha uchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mhe. Abubakar Asenga amekemea vikali vitendo vya ukatili wa kijinsia unoendelea ndani ya jamii yetu dhidi ya wanawake huku akiwataka wanawake hao na wasichana kufika katika ofisi husika 8kiwemo ofisi ya Mkuu wa Wilaya pale wanapofanyiwa vitendo hivyo ili sheria iweze kufuata mkondo wake.
Naye, Mratibu wa Miradi kutoka Shirika la Uswisi Bi. Apaa Mwabena amesema kwa upande wao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake kwenye ufundi stadibi kwa lengo la kuwapatia ajira wanawake hao na kujikwamua kimaisha.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.