Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amethibitisha majengo 7 kujengwa na mengine kufanyiwa ukarabati ambapo itagharimu zaidi ya Tsh. Bil. 41 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kampasi ya Morogoro kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ili kuongeza idadi ya majengo kwa ujifunzaji na ufundishaji wa wanafunzi na wataalam mbalimbali ya kilimo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo Novemba 14, Mwaka huu katika hafla ya utiaji Saini wa mikataba ya ujenzi wa majengo ya chuo cha SUA iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo hicho yakilenga kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Aidha, Mhe. Adam amesema mradi huo utatekelezwa ndani ya miezi 18 pekee na majengo hayo kukamilika kwa ajili ya utoaji huduma ya elimu, hivyo amewataka wakandarasi waliotia saini ya kutekeleza mradi huo kufuata maelekezo ya mikataba na kuhakikisha majengo hayo yanakamilika kwa wakati huku akifurahishwa na wakandarasi wazawa waliotia saini ya mkataba wa ukarabati wa majengo chakavu ya chuo hicho.
“… sote tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa majengo 7 ambapo jumla yake inagharimu Tsh. Bil. 41.05 kukamilisha majengo hayo…” amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amesema chuo hicho kinapaswa kuwa mfano Afrika katika shughuli za kilimo kwa kutumia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mageuzi ya kilimo hapa nchini kwa kuanzia Mkoani humo kuzalisha kutafuta ufumbuzi wa mazao ya kimkakati hususan karafuu, michikichi, parachichi, kokoa na hiriki kwani kilimo ndio uti wa mgongo hapa nchini.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi wa umma pamoja na wananchi waliojiandikisha katika orodha ya daftari la serikali za mitaa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao utahusisha wenyeviti wa mitaa, vitongoji na vijiji ifikapo Novemba 27, Mwaka huu.
Kwa upange wake, Mwakilishi wa Mradi wa HEET Mhandisi Hanington Kagiraki akimwakilisha mratibu wa HEET kitaifa amewahakikishia wakandarasi kuhusu fedha zote za mradi huo zimetayarishwa hivyo hakutakuwa na sababu za kutokamilisha mradi huo kwa wakati.
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda amesema kukamilika kwa mradi huo itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuboresha miundombinu ya kutolea elimu kwani chuo hicho ndio tegemezi katika masuala mbalimbali ya kilimo hapa nchini.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.