Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro inatarajia kutumia zaidi ya Shilingi Bil. 7 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambazo zitatumika kwa ajili ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkoani humo.
Hayo yamebainishwa na Mchumi Mwandamizi Emmanuel Mazengo leo Machi 3 mwaka huu katika kikao cha baraza la wafanyakazi cha Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kilicholenga kupitisha mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Mazengo amebainisha kuwa bajeti hiyo imejikita katika matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo ambayo yatahusisha mishahara kwa wafanyakazi na maslahi ya watumishi.
Aidha, Mazengo amesema kwa upande wa fedha za matumizi ya maendeleo miradi itakayoendelezwa ni pamoja na zaidi ya shilingi Bil. 2.5 zitatumika kwenye ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Fedha nyingine zitatumika kwenye Ujenzi wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya za Gairo, Ulanga na Malinyi lakini pia fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa Ofisi 10 za Maafisa Tarafa zitakazogharimu shilingi milioni 700.
Akifungua kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo, amewataka Wakuu wa Idara, wakuu wa sehemu/vitengo na watumishi wengine kutoa kipaumbele katika kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo kwa mujibu wa maeneno yao ya kazi.
Mhandisi Kalobelo amesema pale ambapo itaonekana kuna tatizo katika kuwapa stahiki zao kwa wakati ni vyema kutoa ushirikiano kwa kuwaeleza sababu ambazo zimepelekea kikwazo cha kutowapa stahiki zao ili kuepuka migogoro baina ya wafanyakazi.
‘’Niwaombe sisi tuliopo hapa wengine ni wakuu wa idara, wengine ni wakuu wa sehemu/vitengo lakini na watumishi wengine, niombe twendelee kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba watumishi wanapata stahiki zao kama inavyotakiwa kisheria, kanuni, taratibu na miongozo ya maeneo yetu ya kazi’’ amesisitiza Kalobelo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Kalobelo amewataka Wakuu wa Idara na Makatibu Tawala wa Wilaya kuepuka malimbikizo ya madeni kwa kuweka mipango mikakati kulingana na pesa wanazopata kikamilifu kila mwezi kutoka Serikali kuu OC hivyo watumie pesa hizo kwa kuzingatia vipaumbele vya mahitaji ya Ofisi zao ili kuepukana na madeni.
Sambamba na hayo, Mhandisi Kalobelo ametoa wito kwa wadau wa kikao hicho kuwa wawezeshaji wa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ipo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na miradi kutoka Serikali kuu na miradi ya Serikali za mitaa.
Akibainisha malengo ya kikao hicho Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Joyce Baravuga amesema ni kuangalia maendeleo na ustawi wa wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro na kupitisha mipango na bajeti ya mwaka 2021/2022 ili ipelekwe Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aidha, Bi. Baravuga amesema amepokea maelekezo ya mwenyekiti wa kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo katika kuzingatia suala la kujali stahiki za watumishi wa chini yao na akatumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa chini yake hususan walimu kusimamia vema mifumo ya elektoniki iliyopo katika shule za Msingi na Sekondari ikiwa ni utekeleaji wa maagizo ya mwenyekiti wa kikao hicho.
Naye, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila ametoa kongole kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya katika kuleta maendeleo katika Mkoa huo, kisha ametoa ombi la kujengewa nyumba au kufanyiwa ukarabati kutokana na miundombinu ya nyumba hiyo kuwa mibovu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.