Zaidi ya shilingi Tsh. Milioni 125 zimepatikana kupitia chakula cha hisani ambapo ilifanyika harambee ya kupata fedha kwa ajili ya maboresho ya miundo mbinu ya Hospitali ya Rufaa ya Morogoro ambayo jana Mei 17 imetimiza miaka 80 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945.
Harambee hiyo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Alhaji Adam Kighoma Malima ambaye alikuwa mgeni Rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika Hoteli ya Morena Manispaa ya Morogoro ambapo wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa huo walichanga fedha taslim na wengine kutoa ahadi na kufikisha kiasi hicho huku Mkuu wa Mkoa naye akiahidi kutafuta Mil. 10
...kwa harambee iliyosomwa leo ningependa isomwe milioni 125 Mkuu wa Mkoa anaenda kujipiga atatoa Tsh. Milioni 10..." amesema Mhe. Adam Malima
Akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro pamoja na wageni waalikwa walioshiriki maadhimisho hayo ya Kilele cha miaka 80 ya Hospitali hiyo Mhe. Kighoma Malima alitumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa Hospitali hiyo ya Rufaa kwa kufanya kazi kwa bidii na nje ya changamoto zozote wanazokutana nazo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Best Magoma amesema Sekta ya afya kwa Mkoa wa Morogoro iko vizuri kutokana na kuwa na Madaktari wenye weledi, wabobevu na wansojituma katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Naye, Dkt. Lita Lyamuya Mganga Mfawidhi mstaafu wa Hospitali hiyo amesema hali iliyopo katika Hospitali hiyo kwa sasa ni nzuri huku akisisitiza kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanatoa huduma bora na yenye kukidhi matarajio ya Serikali na wananchi.
Harambee hiyo ililenga kupata fedha za ukarabati wa miundombinu ya Hospitali hiyo ya Rufaa pamoja na kununulia vifaa tiba kama jitihada za kuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.