Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa reli ya kisasa kipande cha Dar es salaam hadi Dodoma utagharimu zaidi ya Tsh. Trilioni 10 hadi kukamilika kwake.
Dkt. Samia amebainisha hayo Agosti Mosi mwaka huu wakati wa hafla fupi ya ukaguzi wa kituo cha treni cha reli ya kisasa (SGR) cha Morogoro, kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.
Akifafanua zaidi Dkt. Samia amesema wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa reli hiyo katika vipande vingine vilivyobaki hadi kuunganisha nchi Jirani za Burundi, Rwanda na Congo lengo likiwa ni kurahisi usafirishaji wa abiria na bidhaa mbalimbali.
“… tumeweka fedha nyingi kwenye mradi huu kipande cha Dodoma hadi Dar es Salaam ni zaidi ya trilioni 10 zimetumika…” amesema Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Mhe. Samia Suluhu amesema mradi huo ni muhimu kwa jamii kwani unarahisisha usafirishaji na usafirishwaji wa watu na bidhaa ili kukuza uzalishaji mali na kukuza biashara hususan wafanyabiashara katika kuongeza kipato kwa wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Morogoro ni shahidi namba moja kwa kupata mafanikio makubwa ya reli ya SGR kwani mradi huo unatumika kwa wananchi wa aina mbalimbali wakiwemo abiria, wafanyabiashara, watumishi wa sekta za umma na serikali na wengine wengi.
Huduma ya treni ya reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar es salaam hadi Dodoma imeanza tangu Julai 25, Mwaka huu ambapo imezinduliwa hivi leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Huku akiwasisitiza watu kuzalisha kwa wingi mazao ya kila aina ili kukuza uchumi wao kwa kuwa masoko yapo katika nchi hizo ambapo reli hiyo itafika.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.